SIMCU YAJIPANGA KUSHIRIKIANA NA SERIKALI KUTHIBITI WALANGUZI WA CHOROKO

 Na Anita Balingilaki, Simiyu

Chama kikuu cha ushirika mkoa wa Simiyu (SIMCU) kimeiomba serikali mkoani hapo kuendelea kutoa ushirikiano lengo likiwa kuthibiti walanguzi wanaonunua choroko ili  wakulima wauze kwa kutumia stakabadhi ghalani ili waweze kupata tija itokanayo na kilimo.

Ibrahim Kadudu mrajis msaidizi mkoa wa Simiyu akitoa ufafanuzi kwa viongozi wa Amcos

Hayo yamesemwa jana na makamu mwenyekiti wa SIMCU Emmanuel Mwelele wakati akitoa taarifa ya ununuzi wa mazao mchanganyiko kupitia vyama vya ushirika vya msingi (AMCOS) mkoani hapo na kuongeza kuwa wanunuzi wote wa choroko wanunue kupitia mfumo wa mnada na sio kwenda kwa mkulima moja kwa moja.

Aidha ameongeza kuwa chama hicho kilianza utaratibu wa ukusanyaji na kuteua maghala manne ambayo ni Mahaha,Ngulyati,Dutwa na Mwanhuzi huku akisisitiza kuwa changamoto mbalimbali zilikuwepo ikiwemo baadhi ya wakulima wa choroko  kutokuwa na   elimu ya mfumo huo  hatua iliyopelekea zoezi hilo kutofanikiwa kwa kiwango kikubwa.

"Chama kikuu kilipata changamoto ya wakulima ambao hawakuwa na elimu juu ya mfumo huo wa stakabadhi ghalani na walikuwa wakihitaji kupewa pesa taslimu pindi wafikishapo choroko ghalani " aliongeza 

Mwelele alifafanua kuwa  msimu uliopita chama hicho kilipata changamoto nyingine ya usafirishaji wa choroko kutoka kwenye vyama vya msingi na kuzipeleka ghala kuu na kupitia taarifa yake amesema kwasasa wamejipanga na watakuwa wanakodi magari kwaajili ya kusomba choroko.

Akizungumzia maandalizi ya ukusanyaji na ununuzi kwa msimu wa 2021 chama hicho kimeandaa vifungashio 10,000 kwaajili ya kuanzia na vitagawiwa kwenye AMCOS wanachama ,kukutana na wakulima ,watendaji wa vijiji na kata na kutoa elimu juu ya mfumo wa stakabadhi ghalani.

Baadhi ya washiliki wa mkutano huo wakisikiliza kwa makini
Hata hivyo amesema SIMCU imejipanga kuwashirikisha  wakuu wa wilaya zote mkoani hapo kwenye ufunguzi wa mnada wa choroko huku akiongeza kuwa maghala yaliyotumika kukusanya pamba ndio yatatumika kukusanya choroko wakati ikisubiri mnada.


Awali akifungua kikao hicho katibu tawala mkoa wa Simiyu Mariam Mmbaga alisema serikali itaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Amcos na kuyataka mabenki kuzunguka ili kujua idadi ambayo haijafungua akaunti ifunguliwe na penye marekebisho yafanyike na ikiwezekana waweke mawakala maeneo ambayo ni vigumu wao (mabenki) hawafikiki kirahisi.

"mnaweza kuweka mawakala wenu maeneo ya vijijini na tumieni vijana wetu ili wapate fursa ya ajira ,na mnaweza hata kuzitumia Amcos zetu kuwa sehemu ya mawakala wenu "alisema Mmbaga. 

Nae naibu mrajis wa vyama vya ushirika usimamizi na udhibiti wa tume ya maendeleo ya ushirika Collins Nyakunga alisema hadi kufikia desemba 31,2020  maadhimio yote yawe yametekelezwa ambayo ni pamoja na wakulima wote kuwa na akaunti, uwepo wa vitabu vya kumbukumbu ili kujua namna ya uendeshaji wa zoezi hilo sambamba na utolewaji wa elimu ya  namna ya kujaza vitabu hivyo.

Awali mrajis msaidizi wa mkoa wa Simiyu Ibrahim Kadudu alisema msimu uliopita choroko haikuweza kuuzwa kwa mfumo wa mnada kutokana na sababu mbalimbali huku akiongeza kuwa kwasasa maandalizi yameanza mapema hivyo wakulima waibebe dhana hiyo ambayo itawawezesha kulima kwa tija kwani ufumbuzi wa soko/bei umeshapatikana. 

Mariam julias ni katibu wa Amcos ya Ibumba (Itilima) na Edward Wilson ni katibu wa Amcos ya mwafumbuka (Maswa ) wamesema awali idadi kubwa ya wakulima walijua kuuza kwa njia ya stakabadhi ghalani ni wizi lakini sasa jamii hiyo tayari inauelewa japo elimu zaidi inahitajika.

              MWISHO

Post a Comment

0 Comments