TFS YAANZA MWAKA 2021 KWA KISHINDO CHA UTALII .

Na Shushu Joel, Kisarawe. 


Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania  (TFS)umeanza mwaka 2021 kwa kuratibu ziara ya Utalii ikolojia katika Hifadhi ya Msitu wa Mazingira asilia Pugu Kazimzumbwi leo tarehe 4 Januari 2021.

Picha ya pamoja ya wafanyakazi wa TFS mara  baada ya kazi elekezi

Katika ziara hiyo ya aina yake, Mshindi wa Mashindano ya Ulimbwende maarufu Miss Tanzania Rose Manfere na Washiriki wenzake kadhaa wameweza kufika katika Hifadhi ya Msitu wa Mazingira asilia Pugu Kazimzumbwi na kufanya matembezi ya kitalii katika maeneo mbalimbali. 


Ziara hiyo iliyoratibiwa na TFS kwa kushirikiana na Bodi ya Utalii Tanzania(TTB)imeanzia Makao makuu ya TFS Mpingo house jijini Dar es salaam na kuelekea kisarawe ambapo kituo cha kwanza kilikuwa kona ya Bwawa la Minaki ambapo matembezi kwa miguu yalianza na kupitia Bwawa la Minaki na kuzungukia camp mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupiga picha za kitalii. 


Kwa uongozi wa Waongozaji wa Watalii kutoka TFS Kisarawe, Watalii hao wa ndani wameweza kuuliza maswali mengi na kupatiwa majibu kuhusu Uhifadhi wa Misitu na Utalii Ikolojia katika Hifadhi ya Msitu wa Mazingira asilia Pugu Kazimzumbwi. 


Awali akiwakaribisha watalii hao, Anna Lauwo ambaye ni Afisa Masoko kutoka TFS aliwahakikishia kuwa Eneo walilotembelea ni Fursa nzuri kwa vijana kutembelea. 


"Kuna vitu vingi sana hapa vya kufurahia, milio ya ndege, hewa nzuri kabisa, sehemu za kupumzika, sehemu za kufanyia ibada, Michezo ya mitumbwi lakini zaidi ni kufahamu aina mbalimbali za miti asilia, kwa hiyo hapa ni eneo lenye fursa nyingi kwa vijana kutembelea "Lauwo. 


Warembo hao wakiongozwa na Mratibu wa Mashindano ya Miss Tanzania Basila Mwanukuzi wameonyesha vipaji vya kuimba na uwezo mkubwa wa kujiamini katika kufanya kile wanachokiamini.


"Siyo urembo tu, hapa vipaji vimejaa, wanaimba sana tena kwa kujiamini "Basila.


TFS imeaandaa safari hiyo ya Utalii ikiwa ni juhudi za kutekeleza maagizo ya Serikali ya awamu ya Tano kuongeza idadi ya watalii katika Vivutio vya Utalii vinavyosimamiwa na Wakala. 


Huu ni utaratibu uliowekwa kwa Taasisi za Maliasili zibazoshiriki Maonesho ya Circus Mama Africa yaliyofanyika Viwanja vya JWTZ Masaki 22/12/2020 na kufikia Kilele 04 /01/2021 ambapo kila taasisi ilipaswa kupeleka watalii katika moja ya Vivutio vya Utalii inavyosimamia

Post a Comment

0 Comments