Na Omary Mngindo, Mlandizi
WATOTO wanaoishi katika mazingira hatarishi wanaolelewa kwenye Kituo cha Masjid Nour kilichopo Kitongoji cha Mtongani Halmashauri ya Kibaha Mkoa wa Pwani, wamenusurika kuteketea kwa moto.
![]() |
Mbunge wa Jimbo la Kibaha vijijini Michael Mwakamo akizungumza na viongozi nwa eneo hilo mara baada ya kufika katika eneo hilo. |
Moto huo uliozuka kituoni hapo Machi Mosi saa tatu asubuhi, mpaka Waandishi wanaondoka kituoni hapo chanzo chake hakijafahamika, ambapo hata hivyo hakuna mtoto ambe amejeruhiwa kufuatia tukio hilo.
Akielezea mkasa huo mbele ya Mbunge wa Jimbo la Kibah Vijijini mkoani hapa Michael Mwakamo, mmoja wa viongozi kituoni hapo Seif Wenge alisema kwamba akiwa ofisini kwake katika soko la Mlandizi alipigiwa simu akijulishwa rukio hilo ambalo lilidhibitiwa na wananchi waliotumia maji.
"Tunashukuru hakuna madhara kwa watoto wetu 31 wote salama, lakini kuna mtoto mmoja amefika hapa wiki mbili zilizopita akitokea Soga ambae tangu kutokea kwa moto huo mpaka sasa hajaonekana, wenzake wote wale pale, tumetoa taarifa Ustawi wa Jamii pamoja na Kituo cha Polisi Mlandizi," alisema Wenge.
Akizungumza baada ya taarifa hiyo Mwakamo alianza kumshukuru Mwenyeezimungu kwa kutokuwepo madhara kwa wanafunzi hao huku akiwashukuru wananchi wote waliojitokeza kusaidia kuzima moto huo, pia amewapongeza viongozi kwa hatua za haraka za kununua magodoro watayoyatumianafunzi hao.
![]() |
"Tushukuru kwa kutokuwepo madhara ya wanafunzi kwani kikubwa ni uhai, umesema wanafunzi wa kiume ndio wameathirika zaidi kwa kuunguliwa nguo zao na kwamba tayari kuna wahisani wameshakuja kuleta baadhi ya nguo nuwaombe wengine wajitokeze kusaidia vijana wetu," alisema Mwakamo.
Alimtaka mwakilishi wa ofisi ya Mkurugenzi kwenda kuangalia kama kuna uwezekano wa kusaidia kituo hicho wafanye hivyo, huku akiongeza kwamba hicho na vingine vina msaada mkubwa kwa Serikali kwani kunapotokea kupatikana watoto wanaookotwa hupelekwa kwenye vituo hivyo.
"Hivi vituo vina msaada mkubwa kwa Serikali kwani tunapopata watoto tunawaleta katika vituo hivi, hivyo panapotokea maafa kama haya hatuna budi kujitokeza kusaidiana kupambana na maafa yanayowakumba," alisema Mwakamo.
MWISHO.
0 Comments