ACHENI VYOMBO VYA DOLA VIWASHUGHULIKIE HAWA WATU

Julieth Ngarabali,  Chalinze

Wazazi na Walezi mkoani Pwani wametakiwa kuwalinda watoto dhidi ya watu wanaowafanyia vitendo vya ukatili wa kijisia ikiwemo  ubakaji na kuwapa mimba kwa kuacha tabia ya kuingia makubalino na waovu hao na badala yake waache vyombo vya sheria ziwashughulikie wahusika 

Baadhi ya wanafunzi wa shule ya msingi Visezi Vigwaza Chalinze wakiimba wimbo wa Taifa kabla ya kuingia darasani .

 Akizungumza kuhusu matukio ya ukatili , Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema moja ya baadhi ya mambo yanayosababisha changamoto hizo hasa mimba kuendelea ni baadhi ya wazazi kuingia makubaliano na watuhumiwa ili wasichukuliwe hatua za kisheria hali ambayo inafanya  kushindwa kukosekana ushahidi wa kutosha

“Idadi ya watoto wa kike wanaopata mimba ni kubwa wakiwemo wa shule za msingi mfano mwaka jana tu walikuwa 266 mkoani Pwani hivyo jamii inapaswa kuwalinda watoto dhidi ya vitendo kama hivi ambavyo ni vya ukatili ili visiendelee kwani hatua kali ndizo zitakazosaidia kupambana na watu hawa ambao wanakatisha ndoto za watoto wetu,”alisema Kunenge.

Amesema wazazi wanapaswa kukubali watoto wao walelewe na jamii kwani kuna baadhi ya wazazi hulalamika endapo watoto wao wakiadhibiwa na walimu au jamii pale wanapokuwa wamefanya makosa kwani mtoto ni wa jamii hivyo kuadhibiwa ni sehemu ya kurekebishwa .

“Watoto wetu wanapaswa kulindwa na baadhi ya wazazi hasa wale wa kiume wanasema kuwa mtoto wa mwenzio ni mkubwa mwenzio hili jambo siyo sahihi kwani mtoto wa mwenzio ni wako fikiria kama ni mwanao anafanyiwa vitendo vya ngono utajisikiaje hivyo wazazi lazima tuwe walinzi wa watoto,”amesema Kunenge.

Naye  mtoto Irene Mbawala wa Chalinze kwa niaba ya wenzake  amesema  moja ya changamoto wanazozipata ni pamoja na migogoro ya familia, umbali wa shule wanazosoma, matunzo ya watoto, kukosa haki zao za msingi yakiwemo mahitaji muhimu na vitendo vya ukatili.

Mbawala ameiomba jamii kuwasimamia watoto bila kujali ni wa nani ili waweze kupata elimu bora na pia kuwawekea mazingira mazuri ya kusoma.

Naye mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania KKKT Jimbo la Chalinze Mchungaji Joseph Chuma ameongeza kuwa  suala la mimba baadhi ya wazazi wanawaficha watuhumiwa kutokana na mahusiano waliyonayo baadhi wanakuwa ni ndugu hivyo wanapaswa kutowafumbia macho watuhumiwa ili kupunguza vitendo hivyo.

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments