MRADI WA MAJI SAPIWI WAZINDULIWA NA MWENGE WA UHURU


SIMIYU.

WAKAZI wa Vijiji vya Sapiwi na Mwandama wilayani Bariadi Mkoani Simiyu wameipongeza serikali kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Kwa kutekeleza Mradi wa Maji safi na salama ambao umekuwa suluhisho la tatizo la Maji katika maeneo hayo.

Mradi huo ambao imejengwa kwa thamani ya Shilingi Mil. 769, unatarajia kunufaisha watu zaidi ya 6000 na kuwaondolea adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta huduma ya maji ambayo hayakuwa safi na salama.

Akizungumza wakati akisoma taarifa ya Mradi huo, Meneja wa RUWASA wilaya ya Bariadi, Mhandisi Moses Mwampunga amesema kuwa mradi huo umekamilika na unatoa Maji kwa wananchi.

Meneja huyo amewataja ,wananchi kulinda miundombinu ya Maji ili iweze kutumika Kwa muda mrefu na kunufaisha wananchi kama ilivyokusudiwa.

"Mradi huu umetekelezwa kwa gharama ya shilingi Mil.769 na umelenga kunufaisha wakazi 6000 kutoka vijiji vya Sapiwi na Mwandama" amesema.

Kwa upande wao wananchi wameipongeza serikali kwa kutekeleza mradi huo ambao umetatua kero ya Maji kwa wananchi hao ambao awali walikuwa wanatumia Maji yasiyo safi na salama na walikuwa wakichangia na mifugo.

Peter Zabron, Mkazi wa Sapiwi anaishukuru serikali kwa kutekeleza mradi huo ambao imeleta faraja kwa wananchi kwani awali walikuwa wanaugua magonjwa kutokana na matumizi ya Maji Machafu.

 Akizungumza mara baada ya kukagua na kuzindua Mradi huo, kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2025, Ismail Ussi amewapongeza Wananchi kwa kukubali kupokea Maendeleo ikiwemo Mradi huo wa Maji ambao umelenga kutatua shida na changamoto ya Maji katika eneo hilo.

Amesema kuwa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wana jukumu la kusambaza maji ambapo wamefanya kazi kubwa ya kutekeleza miradi ya Maji kutokana na serikali kutoa fedha,

"Wananchi wanamuunga mkono Rais Dkt. Samia, tumeelezwa kuwa walikuwa wakipata changamoto ya Maji safi na salama, wanayapata Maji umbali mrefu, leo serikali imetekeleza mradi huu na unatoa maji...RUWASA imeondoa changamoto ya maji, hongereni sana" amesema Ussi.


Kiongozi huyo amewataka wananchi kuendelea kulinda miundombinu ya Maji na kusisitiza kuwa wasitokee Watu wakaharibu miundombinu hiyo ya Maji na badala yake kila mmoja alinde Mradi huo.

 Mwisho.

Post a Comment

0 Comments