Na Anita Balingilaki,Simiyu
Jumla ya wateja 5253 sawa na 51% wanaohitaji usaidizi wa masuala ya kisheria wamefikiwa mkoani Simiyu kutoka kwa wasaidizi wa kisheria wanaosimamiwa na Kawiye Social Development Foundation (KASODEFO) chini ya ufadhili wa Legal Services Facility (LSF).
![]() |
| Afisa ufatiliaji na tathimini kutoka KASODEFO John Titus akitoa taarifa ya kipindi cha miaka minne ya utekelezaji wa mradi ambao umeisha muda wake |
Hayo yamesemwa na afisa ufatiliaji na tathimini wa kutoka KASODEFO John Titus wakati akitoa taarifa ya kipindi cha miaka minne kwenye kikao cha kufunga mradi wa kuimarisha upatikanaji wa haki kupitia msaada wa kisheria endelevu na kuongeza kuwa awali malengo yalikuwa kuwafikia wateja 3500 lakini wakaona idadi ni ndogo ikaongezwa hadi 9804 huku akifafanua kuwa kesi zinazoongoza kuwafikia wasaidizi wa kisheria mkoani hapo ni migogoro ya ardhi.
"matokeo haya ni baada ya jamii kupata uelewa na kuanza kutoa taarifa zamani watu walikuwa wanamalizana chini kwa chini lakini baada ya kupata uelewa wanatoa taarifa kwenye vyombo husika ukiangalia kesi tulizozipokea..migogoro ya ardhi 981,mirathi 814, migogoro ya ndoa 765, matunzo ya watoto 505 na madai 844 na hizi kesi ni zile zilizofika kwa wasaidizi wa kisheria lakini mkumbuke tunavyo vyombo vingine vya kisheria na mabaraza kwahiyo zingine zilipelekwa huko kikubwa hapa tuwaombe wasaidizi wa kisheria wajikite zaidi kutoa msaada wa kisheria "alisema Jonh .
Marius Isavika ni meneja miradi kutoka KASODEFO amesema kwa kipindi cha miaka mitano wamefanikiwa katika nyaja tofauti ikiwemo utoaji wa elimu, msaada wa kisheria,kuziimarisha taasisi za wasaidizi wa kisheria pamoja na kuboresha mahusiano baina ya wasaidizi wa kisheria na serikali.
![]() |
| Aliyesimama ni msajili msaidizi wa taasisi zinazotoa huduma za msaada wa kisheria kutoka wilaya ya Maswa Elizabeth Mushi |
"kwa kipindi cha miaka minne tumetoa elimu ya sheria kwa 106% ,tumetoa msaada wa kisheria kwa 51% ,tumeziimarisha taasisi za wasaidizi wa kisheria lengo likiwa waweze kujisimamia baada ya mradi kuisha na tumeboresha mahusiano baina ya wasaidizi wa kisheria na serikali "alisema Isavika
Mbali na hayo Isavika amezitaja changamoto walizokutana nazo kwa kipindi cha miaka minne kuwa ni pamoja na baadhi ya wasaidizi wa kisheria kuhama /kuacha kazi,uwepo wa idadi ndogo ya wasaidizi wa kisheria ikilinganishwa na wingi wa kata na mwitikio mdogo wa jamii.
Akijibu namna walivyokabiliana na changamoto hizo Isavika alisema walitoa mafunzo kwa watoa huduma wapya ili kufidia wale waliohama / kuacha kazi, sehemu (kata) ambazo hazikuwa na watoa huduma KASODEFO ilifika kutoa elimu na kuhusu jamii kutokuwa na mwitikio walitumia viongozi na wazee wenye ushawishi hatua iliyopelekea badae kuwa na mwitikio mkubwa tofauti na awali ambapo jamii ilishindwa kuwa na imani ya huduma kwa madai kuwa kwanini itolewe bure bila malipo yoyote .
Aidha Isavika aliongeza kuwa matarajio ya KASODEFO ni kuona vituo vya wasaidizi wa kisheria vikiendelea kutoa huduma baada ya mradi huo kuisha na changamoto za ukatili wa kijinsia na migogoro ya ardhi vikipungua au kuisha kabisa.
Nao baadhi ya wasajili wa wasaidizi wa taasisi zinazotoa huduma za msaada wa kisheria wa wilaya akiwemo Elizabeth Mushi kutoka halmashauri ya wilaya ya Maswa na Amina Mbwambo kutoka halnashauri ya wilaya ya Itilima wamesema ni vema shughuli za wasaidizi wa kisheria zikaunganishwa na shughuli/matukio ya kila siku huku wakiongeza kuwa haijalishi uchache uliopo wa wasaidizi wa kisheria.
"mfano mzuri sisi Maswa mara nyingi tunapoenda kukutana na vikundi vya kinamama,vijana na watu wenye ulemavu mara nyingi tunaambatana na wasaidizi wa kisheria na tunaamini idadi kubwa itapata elimu na hatimaye kuifikisha mbali zaidi na hatua hiyo inasaidia kuongeza uelewa wa masuala ya kisheria" alisema Mushi.
Kwa upande wao baadhi ya wasaidizi wa kisheria wameahidi kufanya kazi kwa bidii katika kuisaidia jamii huku wakiiomba KASODEFO kuendelea kutoa msaada pale watakapoweza ikiwa ni sambamba na kuwaunganisha na mashirika mengi ili waweze kuendelea kufanya kazi zao kwa ufanisi kama ilivyokuwa kipindi cha chote cha mradi.
Akifunga kikao cha kufunga mradi huo ,msajili msaidizi wa taasisi zinazotoa huduma za msaada wa kisheria kutoka mkoa wa Simiyu Fadhili Wilhem ameipongeza KASODEFO kwa kiasi milioni 160 ilichokitoa kwa kipindi cha miaka minne kwa taasisi tano zinazojihusisha na masuala ya usaidizi wa kisheria mkoani hapo ambapo kila taasisi ilipokea kiasi cha shilingi milioni 8 kwa mwaka huku akizitaka taasisi hizo kuendelea kufanya kazi kwa kuzingatia sheria za nchi na lengo likiwa kuisaidia jamii kwenye mambo ya kisheria ili ipate haki zao kwa kufuata utaratibu sahihi.
...mwisho...



0 Comments