MARIAM AWATAKA WANAWAKE KUTORUDI NYUMA

Na Shushu Joel,Kibaha

 WANAWAKE wilayani Kibaha wametakiwa kutoisubiri serikali kuwafanyia kila kitu badala yake watumie fursa zilizopo kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi na kuacha kuwa tegemezi.

Mkurugenzi wa Kampuni yua Twiga Intertaiment Mariam Ahmed akizungumza na kina mama(NA SHUSHU JOEL)

Hayo yalisemwa mjini Kibaha na mkurugenzi wa kampuni ya Twiga Entertianment Mariam Ahmed wakati wa sherehe za miaka miwili za kikundi cha Pwani Generation Queens (Mwanamke Sahihi).


Ahmed alisema kuwa kuna baadhi ya fursa kwa wajasiriamali zimetolewa kwa wanawake moja kwa moja ambazo ni asilimia nne kutoka mapato ya Halmashauri ambazo hutolewa kupitia vikundi.


“Nyie kweli ni wanawake sahihi kwani mmeunda kikundi ambacho kinawapa uwezo wa kuweza kukopa kwani sifa mnazo na fedha hizi ziko wazi kwa ajili yenu badala ya kusubiri misaada,”alisema Ahmed.

Mkurugenzi huyo ambaye aligombea nafasi ya Ubunge Jimbo la Kibaha Mjini alisema kuwa wanawake wasisubiri kusaidiwa bali wanachotakiwa ni kutumia fursa zilizopo kama za mikopo ya Halmashauri.


“Hakuna sababu ya kukaa ndani mwanamke nawapongeza wote kwani hapa kila mtu anashughuli yake ya kiuchumi huu ni mfano wa kuigwa kwa wanawake wilaya ya Kibaha na mkoa mzima wa Pwani,”alisema Ahmed.


Naye mwenyekiti wa kikundi hicho cha wanawake Betty Msimbe alisema kuwa hadi sasa kikundi chao kina wanachama 41 na katika kipindi cha miaka miwili tangu kuanzishwa wameweza kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 52.7


Msimbe alisema kuwa wanatoa mikopo yenye riba nafuu kwa wanachama wake ambayo ni asilimia tano tu tofauti na taasisi nyingine za kifedha ambazo nyingine hutoza riba hadi asilimia 25.


Alisema kuwa katika kipindi hicho wameweza kugawana kiasi cha shilingi milioni sita ikiwa ni sehemu ya faida waliyoipata huku wakiwa na akiba ya kiasi cha shilingi milioni 79 na pia waliweza kutoa matofali 1,000 kwa kituo cha watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu na kuwatembelea wafungwa magereza.


Mwisho.

Post a Comment

0 Comments