Julieth Ngarabali, Chalinze.
Changamoto ya wanafunzi hasa wa umri wa miaka mitano mpaka nane kutembea umbali mrefu kati ya kilomita saba mapaka 10 kila siku kwenda shule imewakera wanakijiji wa Visezi kitongoji cha Lamboni kata ya Vigwaza Chalinze na kuamua kujenga madarasa ya shule shikizi ili kuwapunguzia adha hiyo watoto hao.
Mwenyekiti wa Kitongoji hicho cha Lamboni Hamisi Amri amesema changamoto ya kutembea umbali huo mrefu imesabaisha pia wanafunzi wengi wa madarasa ya awali kuwa wanalala njiani na kushindwa kumudu masomo kwa uchovu wanapokwenda shule ya msingi ya Visezi iliyopo eneo.
Amesema kutokana na changamoto hiyo wananchi wa eneo hilo sasa wameamua kuanzisha shule shikizi na kuipa jina la Msilale ili watoto wadogo wanaokwenda Visezi waweze kusoma jirani na hapo badala ya kwenda tena mbali
"Wananchi wana ari sana ya elimu lakini tatizo shule zipo mbali na wanaotakiwa kuanza madarasa ya awali ni watoto wadogo sana, mfano hapa tu ilipo shule shikizi yenyewe bado kuna wanafunzi wanatembea km tatu kufika hapa , hivyo kupitia mikutano ya Kitongoji tulianza kuibua ujenzi huu mwaka 2016 kwa michango na nguvu kazi yetu wenyewe tukapata madarasa mawili na sasa tunaomba wadau watuchangie "alisema
Akisoma risala ya shule ya msingi shikizi Msilale Mwalimu Asha Lipala alisema wazo la kujenga lilianza mwaka 2016 na mwaka 2017 walikamilisha madarasa mawili na kuanza na wanafunzi 45 .
Lipala alieleza kuwa kwa sasa shule shikizi hiyo ina jumla ya wanafunzi 100 wa awali, la kwanza , la pili na la tatu na walimu wanne kati yao watatu wa kujitolea ikiwa na lengo kuu la kuboresha elimu kwa kuhakikisha watoto wote wenye umri wa kwenda shule wanapata elimu bora na kwa ukaribu zaidi.
"Kwa sasa wazazi wamefanikiwa kujenga madarasa mawili, ofisi moja, vyoo tundu nane kati yake vinavyotumika vinne , nyumba moja ya walimu na bado tunaendelea na mchakato wa ujenzi vyumba viwili vingine vya madarasa ambapo tumefyetua tofali 2,200 kwa sababu tunatarajia kuwa na darasa la nne mwaka ujao ili shule itimize vigezo vya kusajiliwa, hivyo tunaomba wadau nao watuchangie jamani"alisema Lipala.
Hata hivyo amesema pamoja na jitihada hizo bado wanakabiliwa na changamoto ya upungufu wa madarasa ambapo wanafunzi wanalazimika kusoma kwa shifti na wengine kusomea nje chini ya miti na ikitokea mvua ikanyesha wanakosa pa kukaa, upungufu wa viti, meza, madawati , tanki la kuhifadhia maji, upungufu wa walimu yupo mmoja tu wa Serikali na vifaa vya ufundishaji kwa ujumla.
Awali mmoja wa wazazi Bibi Teresia ameongeza kuwa wao kama wazazi wanaumia kuona watoto wao wadogo wanashindwa kumudu vipindi vya darasani kwa uchovu unaotokana na kutembea umbali huku baadhi wakianza kuchukia kwenda shule wakidhani ni adhabu hivyo kushauri wadau wawachangie ili nao wapate elimu bora.
Mwisho.

0 Comments