Julieth Ngarabali , Pwani
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amewataka Viongozi wa Halmashauri zote na watendaji wa Afya kitengo cha lishe Mkoani hapo kuhakisha Chakula kinapatikana mashuleni.
Kunenge ameyasema hayo katika kikao Kazi cha tathimini ya mkataba wa lishe katika Mkoa wa Pwani kilichofanyika Agosti 4, 2021 mjini Kibaha.
Ameeleza kuwa, lishe bora katika jamii ni kichocheo cha maendeleo endelevu katika nyanja zote na hasa ya viwanda, afya, kilimo, Elimu, biashara na uchumi lakini hayo yatafikiwa endapo athari za lishe duni au utapiamlo zitadhibitiwa au kutokomezwa.
"Hali ya udumavu kwa Mkoa wetu ni 23.8% ukilinganisha na ile ya Taifa 30.1% (TNNS, 2018) ambayo tafsiri yake ni kuwa katika watoto 100 wenye umri chini ya miaka mitano watoto 24 wamedumaa na hata wakiwa watu wazima itakuwa ngumu kwao kuinua uchumi wa familia na taifa kwa ujumla " amesema Kunenge.
Ameongeza kuwa katika kila darasa lenye watoto 45 watoto 11 wanaweza kuwa wadumavu na hawafundishiki hivyo basi, ni vyema tukaona umuhimu wa kusisitiza upatikanaji wa chakula mashuleni.
Amebainisha kuwa upatikanaji huu unaweza kufanyika kwa shule kuzalisha matunda, mboga na mazao ya chakula kama vile mihogo, mahindi na mpunga pia ufugaji wa wanyama wadogo wadogo kama kuku, bata na sungura kulingana na hali halisi ya maeneo ya shule.
Amesema endapo utekelezaji huo utafanyika ni dhahiri kwamba watoto shuleni watakuwa na afya bora na wataweza kuelewa wanayofundishwa.
Hata hivyo Kunenge amezipongeza Halmashauri za Mkoa wa Pwani kwa utekelezaji mzuri wa Mkataba wa Lishe kwa kipindi cha Januari hadi Juni 2021,
Amezitaka Halmashauri ambazo hazijafanya vizuri kutokana na utoaji madogo wa fedha kwa robo ya pili na kutokutolewa fedha za utekelezaji wa shughuli za lishe zilizopangwa kwa robo ya tatu kutoa fedha hizo kwa wakati.
Mwisho.
0 Comments