NA MWANDISHI WETU
AJALI ya moto iliyotokea jana latika mji wa Malampaka wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu imeteketeza vyumba nane vikiwemo vyumba saba vya biashara na chumba kimoja cha kuishi na kuteketeza mali zote.
Mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo ambaye alifika jana eneo la tukio alisema kuwa tukio hilo lilitokea majira ya 1.30 jioni.
Alisema kuwa nyumba hiyo moja yenye vyumba hivyo vilivyoungua ni mali ya Mahela Jilala mkazi wa kijiji cha Bukangilija wilayani humo.
Kaminyoge alisema kuwa chanzo cha moto huo kwa taarifa za awali zinaeleza kuwa mtu mmoja(jina lake halikuweza kupatikana) ambaye ni dereva wa kubeba abiria kwa kutumia pikipiki maarufu kwa jina la bodaboda alikuwa akivuta sigara nje ya duka la Mussa Maliganya ambaye ni muuza mafuta ya Petrolia na disel.
Alisema kuwa ndipo moto ulipolipuka na kuanza kusambaa katika vyumba vingine na kuteketeza mali zote ambazo hadi sasa thamani yake haijaweza kupatikana hadi sasa.
"Baada ya moto kushika kasi ndipo uliposambaa kwenye maduka mengine hadi sasa thamani ya hasara haijaweza kupatikana na kazi inaendelea ili kujua thamani ya vitu vyote vilivyoungua kwenye ajali hiyo mbaya ya moto kutokea kwenye mji huo,"alisema.
![]() |
| Muonekano wa maduka yaliyoungua na moto |
Alisema kuwa mara baada ya moto kutokea mmiliki wa duka lililokuwa likiuza mafuta alitoweka ndipo wananchi wakishirikiana na wafanyakazi wa Kampuni ya Ujenzi ya Kichina ya CCECC inayojenga reli ya kisasa katika mji huo walifanikisha zoezi la kuzima moto huo majira ya saa 3.30 usiku.
Aliongeza kueleza kuwa katika ajali hiyo hakuna madhara yoyote yaliyotokea kwa binadamu.
Baadhi ya wananchi walioshuhudia moto huo ukiwaka waliitupia lawama serikali kwa kuwaruhusu baadhi ya wafanyabiashara kuuza mafuta hao kwenye maeneo yasiyoruhusiwa.
MWISHO


0 Comments