WAZAZI wa wanafunzi wa shule ya msingi Boko Timiza kata ya Tumbi Halmashauri ya Mji Kibaha wameridhia kuchangishana fedha kwa ajili ya chakula kwa watoto wawapo shuleni.
Katika kikao kilichofanyika mwishoni mwa wiki kilichoitishwa na Diwani wa Tumbi Raymond Chokala wamekubaliana kila mzazi kuchangia Sh. 200 kwa siku ili mtoto aweze kupata chakula.
Diwani Chokala aliitisha kikao hicho baada ya maelekezo yaliyotolewa hivi karibuni na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge akielekeza kila shule wanafunzi wapate chakula kuondoa udumavu.
Akiongea baada ya kikao hicho Chokala alisema amelazimika kufanya vikao na wazazi kwenye shule za msingi tano zilizopo katika kata hiyo kushauriana kwa pamoja namna ya wanafunzi kupata chakula wakiwa shuleni
Alisema kuwepo kwa chakula shuleni itaondoa udumavu lakini pia ni njia mojawapo ya kuinua ufaulu kwa wanafunzi.
" Nimeanza na shule ya Boko Timiza hii imekuwa na ufaulu hafifu mambo mengi yanaelezwa kuchangia hilo ikiwemo la mwamko mdogo wa wazazi katika suala la elimu lakini kikao changu cha leo kimekuwa na mafanikio makubwa kwangu na nimetoa sufuria kwa shule hiyo" alisema.
Alisema muitikio ulioonyeshwa na wazazi hao unatoa mwanga wa mabadiliko kuanzia kwenye ufaulu wa mitihani lakini pia wazazi kushiriki moja kwa moja kuwafuatilia wanafunzi.
Alisema sasa wanafunzi wa shule hiyo wataanza kupata chakula lakini pia wamekubaliana wanafunzi waanze kilimo cha viazi lishe eneo la shule kwa ajili yao.
" Tumekubaliana wazazi na walimu wakati wakiendelea na.michango ya kila siku ili wanafunzi wapikiwe chakula shuleni lakini pia wameridhia wanafunzi waanze kilimo cha viazi lishe vitasaidia kuongeza chakula na hakutakuwa na mwanafunzi atakayesoma akiwa na njaa sasa" alisema Chokala
Diwani huyo aliahidi kuendelea na vikao kwenye shule nyingine zilizosalia kuzungumza na walimu na wazazi kuweka utaratibu wa kupatikana kwa chakula shuleni.
Hivi Karibuni Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge alieleza hali ya udumavu kwa mkoa huo kuwa ni asilimia 23.8 ukilinganisha na ile ya taifa ambayo ni asilimia 30.1 (TNNS, 2018).
Alisema tafsiri ya takwimu hizo ni kwamba katika watoto 100 wenye umri chini ya miaka mitano watoto 24 wamedumaa na hata wakiwa watu wazima itakuwa ngumu kwao kuinua uchumi wa familia na taifa kwa ujumla.
Kunenge aliongeza kuwa katika kila darasa lenye watoto 45 watoto 11 wanaweza kuwa wadumavu na hawafundishiki hivyo basi, ni vyema kukawa na umuhimu wa kusisitiza upatikanaji wa chakula shuleni.
"Upatikanaji huu unaweza kufanyika kwa shule kuzalisha matunda, mboga na mazao ya chakula kama vile mihogo, mahindi na mpunga pia ufugaji wa wanyama wadogo wadogo kama kuku, bata na sungura kulingana na maeneo ya shule ili wanafunzi wapewe" alisema.
Alisema endapo utekelezaji huo utafanyika ni dhahiri kwamba watoto shuleni watakuwa na afya bora na wataweza kuelewa wanayofundishwa na kuinua ufaulu kwenye mkoa huo.
Mwisho.
0 Comments