WAZIRI NDUGULILE NA WAZIRI KELEMANI WAJA NA MAPINDUZI

 Na Shushu Joel

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wamesainiana mkataba wa mashirikiano na Wizara ya Nishati kupitia Shirika la Umeme TANESCO  kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya mkongo kwa kutumia miundombinu ya umeme.

Akizungumza katika hafla hiyo Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya habari  Dkt. Faustin Ndungulile amesema utekelezaji wa mkataba huo utasaidia TANESCO kupitisha miundombinu ya umeme kutumia nguzo zitakazokuwa zimejengwa kwa ajili ya miundombinu ya mkongo wa Taifa.

Aidha Dkt Ndungulile amesema awali walikuwa wakichimba mashimo ila kwa sasa wanatumia nguzo ambapo mkongo utapita juu kwenye nguzo ili mawasiliano yawafikie watanzania wote maana ni haki yao ya msingi.

“Nguzo hizi zitajengwa kwa viwango sawa na za sasa za TANESCO na zitajengwa kwa ushirikiano wa pamoja ambapo hii itapunguza gharama za usambazaji wa umeme" Amesema Dkt.Ndungulile.

Kwa upande wake Waziri wa Nishati Medadi Kalemani  amesema mashirikiano hayo ni matokeo ya maelekezo ya Rais Samia Suluh ya kuzitaka wizara zote zifanye kazi kwa pamoja ili kuipunguzia serikali gharama.

Mashirikiano kati ya TANESCO na TTCL  maana yake kuna majukumu ya pande zote mbili yakufanya ikiwemo kuimarisha utoaji huduma kwa jamii

Aidha amewapongeza wataalamu wa pande zote mbili kwa ubunifu waliofanya ambapo amesema ushirikiano huo utapunguza gharama kwa serikali, kuimarisha mahusiano kwa sekta zote mbili na kubadilishana utaalamu na teknolojia na kuwa na miundombinu endelevu.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya habari Zainabu Chaula amesema mkataba huo utaboresha makubaliano ili kuleta tija ya uwekezaji na matumizi ya pamoja ili kuhakikisha kasi ya uwekezaji wa miundombinu ya mawasiliano inaongezeka na gharama zinapungua.

MWISHO



Post a Comment

0 Comments