REHEMA KAWAMBWA BINTI ANAYETUMIA KALAMU NA UBUNIFU KULETA MABADILIKO CHANYA KATIKA JAMII

NA MWANDISHI WETU

Uandishi wa vitabu ni njia adhimu ambayo hutumika huakisi mambo mbalimbali yatokeayo katika jamii husika kwa lengo la kuelimisha, kukemea, kuburudisha n.k ili kuleta mabadiliko chanya kwa jamii husika.

Rehema Kawambwa akifurahia jambo na baadhi ya wanafunzi mara baada ya kuwatembelea wanafunzi hao. 

Duniani kote inaelezwa kuwa maandishi ndio hufanikisha sekta nzima ya elimu, ambapo usomaji wa vitabu husaidia watoto 

kujifunza mambo, na kuwa na juhudi kujiandalia maisha ya baadae.

  

Katika makala hii inamuelezea Rehema Kawambwa, msichana ambae ni mwandishi wa vitabu hasa vya watoto, mshairi, na Katibu wa Mbunge Viti Maalum (Mhe. Subira Mgalu), kutoka mkoani Pwani.


Rehema anasema uandishi wa vitabu pamoja na majukumu mengine kwake havijawahi kuwa shida, kwani anapangilia vema muda wake.


Mpaka sasa ameweza kuandika vitabu viwili; vikiwemo kitabu cha mashairi kiitwacho SOUND OF WISDOM (SAUTI YA BUSARA), na kitabu cha watoto kiitwacho ZAWADI YA WINO (BARUA KWA WATOTO) alichoshirikiana na waandishi wengine wanne kutoka nchini Tanzania, na Ujerumani.


Rehema anasema, uandishi wa vitabu mbali na kuwa na faida katika mauzo ya nakala, lakini kwa upande wake ni kitu ambacho anapenda kukifanya kutoka moyoni, na ndio sababu mashairi yake mbalimbali huyaandika kwa hisia kuviwakilisha vile avionavyo kwenye jamii.


KURATIBU WOCHIPODA

Bi. Gloria Gonsalves, ambaye ni mwandishi wa vitabu na mashairi aishie nchini Ujerumani, ambaye pia ni Mwanzilishi wa Siku ya Ushairi wa Watoto Duniani ambayo hufanyika kila Jumamosi ya kwanza, ya mwezi Oktoba kila mwaka kuanzia mwaka 2014 (WoChiPoDa - World Children's Poetry Day), anasema alivutiwa sana na uandishi wa Rehema kupitia mitandao ya kijamii, ijapokua hawajawahi kuonana ana kwa ana lakini aliyapenda maandiko yake, na jinsi anavyojitoa kwa jamii, hayo yote yalimjengea imani na mnamo mwaka 2018 aliweza kumchagua kuwa Mratibu wa maadhimisho ya siku hiyo kwa Mkoa wa Pwani.


"Nilifarijika kupata nafasi hiyo hasa kwa mkoa ambao ninaishi kwa kuwa niliona nimepata fursa ya kuwapa motisha, morali na ari watoto kupenda kusoma, pamoja na kujifunza uandishi wa mashairi kwa lengo la kuwajenga kuwa waandishi wazuri katika maandiko yao kwa baadae," Rehema anasema.


REHEMA KAWAMBWA NA JAMII

Tofauti na shughuli za Uandishi kwa ujumla, Rehema anasema hujishughulisha na mambo ya kijamii tangu mwaka 2009 hasa kusaidia mambo ya kielimu, na kiafya kwa watoto, wanawake na wazee wasiojiweza katika mikoa mbalimbali nchini, na aliamua asianzishe Taasisi binafsi, bali akaona shughuli hizo azipe jina maalum la Rehema Kawambwa Na Jamii.


MRADI WA UTALII KISARAWE NA PWANI PAZURI

Rehema anasema amekuwa akipenda kufanya vitu kwa jamii kwa kuacha alama, hivyo tofauti na kazi za kijamii na maandiko yake katika vitabu ameanzisha Mradi wa kutengeneza T-shirts alizozipa jina la UTALII KISARAWE ambazo amelenga kuvitangaza vivutio vya Utalii vilivyopo wilayani Kisarawe, pia T-shirts za PWANI PAZURI ambazo amezipa picha inayoakisi baadhi ya vitu vilivyomo mkoani Pwani, kwa dhumuni la kuutangaza mkoa huo ndani na nje ya nchi, pamoja na vivutio vya utalii na vitu vyote vizuri vilivyopo mkoani humo.


Rehema anatoa rai kwa waandishi wa vitabu kuwa lazima wajipe muda ili kupata marejeo muhimu, yatakayo wasaidia katika maandiko yao. 

Pia, kutambua njia muhimu na zilizo bora kuzitumia katika kukuza na kuendeleza mawazo yao ambayo huwasilishwa kwa hadhira kupitia maandishi ambayo huchangia kubadilisha, na kupitisha maarifa kutoka kizazi kimoja mpaka kingine, ama kutoka jamii moja hadi nyingine.


Kwa ujumla, waandishi wa vitabu na maandiko mbalimbali wana athari na ushawishi mkubwa kwa jamii, hii inatokana na maandiko mbalimbali yatokanayo na utafiti. Uandishi ni njia nzuri inayopelekea kufanikisha sekta ya elimu na uhifadhi wa amali mbalimbali na utamaduni wa jamii kwa kuacha alama kupitia maandishi, ukizingatia kwasasa uandishi ndio unaoshika hatamu hususan katika mitandao mbalimbali ya kijamii kulinganisha na masimulizi.

Post a Comment

0 Comments