BIASHARA YA NGONO,MILA POTOFU,NGOMA ZA USIKU ZATAJWA CHANZO CHA VVU

 Julieth Ngarabali, Kibiti

Biashara ya ngono, mila potofu katika jamii, ndoa za utotoni , ulevi wa kupindukia, ngoma za usiku pamoja na kuwepo kwa maeneo hatarishi ya starehe yametajwa kuwa ni miongoni mwa sababu zinazoendelea kuchangia maambukizi ya virusi vya Ukimwi VVU.

Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Ahmed Abas akizungumza na wananchi kuhusu kila halmashauri kuendelea kutoa elimu ya Virusi vya ukimwi

Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Mkoani Pwani Ahmed Abass amesema kutokana na changamoto hiyo viongozi ngazi zote wanaopaswa waendelee kutoa elimu ya kujikinga na maambukizi ya VVU na Ukimwi ili kutengeneza mazingira ya mtu mmoja mmoja kujitambua zaidi.

Pia hata shuleni wanafunzi wawe wanapewa elimu ya namna ya kujikinga na maambukizi kwa sababu kundi hilo nalo lipo hatarini kupata maambukizi kupitia njia ya kushea vitu ikiwemo viwembe.

"Hali sio nzuri sana  maana adi kufikia Novemba 20 mwaka huu wa 2020/2021 tumeambiwa na wataalamu wetu wa ngazi ya mkoa kuwa jumla ya watu wanaoishi na VVU walioandikishwa ni 47,754 kati yao waliopo  katika matumizi ya dawa ni 46,634 wakiwemo pia na watoto sawa na asilimia 98 ya walioandikishwa  "amesema Abass

Ameshauri  jamii kuwa na matumizi sahihi  dawa za kufubaza VVU , ARV'S kwa sababu zimethibitishwa zinasaidia kuvubaza wadudu au Ukimwi na hivyo kila Halmashauri iendelee kutoa pia elimu ya ufuasi mzuri wa dawa hizo na matumizi sahihi ya kinga.


Naye mwenyekiti wa Baraza la watu wanaoishi na VVU na Ukimwi wilayani humo ( KONGA) Bakari  Mnangi amebainisha kuwa wanapinga tabia ya  unyanyapa na ubaguzi mbalimbali wanaofanyiwa watu wanaoishi na ugonjwa huo kwani hakuna hata mmoja aliyewahi kusema alipenda kuupata ana aliufata makusudi hivyo ionekane ni maambukizianayopata mtu kama ilivyo kwa maradhi mengine


Bakari ameongeza kuwa Baraza hilo lina changamoto ya ukosefu wa rasilimali fedha tatizo ambalo linawakwamisha kutoka eneo moja kwemda jingine vijijini kwenye kata kutoa elimu kuhusu uhalisia wa VVU kwa sababu wao wanajua maana wanaishi navyo.


"Tunashindwa kuzikifikia kata zetu 16 zilizopo Kibiti kwa sababu hatuna usafiri wala fedha , tunatamani kila mara tuwe tunakutana na jamii kwenye hizi kata tuwaelimishe kuhusu huu ugonjwa  ili kuondoa maambukizi mapya na unyanyapaa "amesema Bakari.


Mwisho.

Post a Comment

0 Comments