Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis
Hamza Khamis ametoa rai kwa wafugaji nchini kuzingatia hifadhi ya mazingira
kwa kutoharibu vyanzo vya maji.
Ametoa rai hiyo wakati wakati wa Kongamano la Wadau
Sekta ya Mifugo lililofanyika jijini Dodoma na kufunguliwa na Waziri Mkuu Mhe.
Kassim Majaliwa.
Amesema kuwa kwa mujibu wa utafiti wa kimazingira, sehemu kubwa ya
uchafuzi wa mazingira inatokana na shughuli za kibinadamu zikiwemo kilimo
kisicho endelevu, ufugaji usio endelevu na uchimbaji wa madini usiofuata sheria
za mazingira.
Mhe.Khamis amesema pamoja na kuwa ufugaji ni sekta kubwa inayokuza
uchumi na kutangaza nchi yetu wafugaji wanao wajibu wa kuhakikisha
wanafuata sheria za mazingira.
“Niwaombe ndugu zangu wafugaji tuhakikishe hatuchungi wala hatunyweshi maji
mifugo yetu kwenye vyanzo vya maji kwani kwa kiufanya hivyo tutasababisha
uharibifu wa mazingira na kuua viumbe waishio humo,” aalisema.
Aidha, naibu waziri huyo amewasisitiza wafugaji na wananchi kwa ujumla
kupanda miti na kuitunza ili kusaidia kupambana na athari za mabadiliko ya
tabianchi yanayoikumba nchi yetu.
Amesema hali ni mbaya kwasababu maeneo mengi wananchi wamekata miti
ovyo hali inayosababisha ukosefu wa mvua na hivyo ukame kukithiri katika
maeneo mbalimbali ya nchi.
Naibu Waziri Khamis amesema kuwa mifugo inahama kutafuta malisho
kwasababu ukame unaosababishwa na ukosefu wa mvua uliochangiwa na
ukataji miti.
“Wakati tunapita na Kamati ya Mawaziri tumeona baadhi ya maeneo
yameakauka sana kwa sababu za kibinadamu zikiwemo kilimo, ufugaji au
uchomaji moto ovyo kwa ajili ya kuni na mkaa, niwashauri ndugu zangu pamoja
twendeni tukapande miti na kuishughulikia (kuitunza),” alisisitiza
0 Comments