Na Shushu Joel, Bukombe
VIJANA wa Jimbo la Bukombe Mkoani Geita wamempongeza Mbunge wa jimbo hilo ambaye ni Waziri wa Nishati na Naibu Waziri Mkuu kwa ujenzi wa chuo cha Veta katika kijiji cha Bulangwa wilaya ya Bukombe.
![]() |
NAIBU Waziri Mkuu Dkt Dotto iteko akifuatilia jambo kwa umakini katika moja ya shughuli zake za kila siku anazozifanya. |
Wakizungumza kwa hisia na Mwandishi wa HABARI MPYA MEDIA Vijana hao walisema kuwa kile kilio cha muda mrefu kinakwenda kumalizika katika wilaya ya Bukombe.
Alex Marcel ni Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UVCCM) kata ya Bulangwa alisema kuwa uwepo wa chuo hicho kinaenda kuwa suluhisho la ajira kwa vijana kwani wanakwenda kupata ujuzi wa aina mbalimbali na hivyo kupelekea wengi wao kuwa na ajira za uhakika.
Aidha Alex aliongeza kuwa kukamilika kwa VETA hiyo ni neema kubwa kwa vijana wa Bukombe kwani Bukombe inakwenda kuwa na Viwanda vidogovidogo Vingi hivyo ajira nyingi zinakwenda kutengenezeka wilayani Bukombe.
"Nimpongeze sana Mbunge wetu Mhe Dkt Dotto Biteko kwa jinsi ambavyo amekuwa mbunifu wa kutatua changamoto za ajira kwa wananchi wa Bukombe kwani kukamilika kwa VETA hii inakwenda kutatua ajira kwa vijana" Alisema Mwenyekiti huyo wa Vijana kata ya Bulangwa Ndugu Alex.
Naye Mmoja wa wazee maarufu wa wilaya ya Bukombe Alexander Mtuzya (81) alisema kuwa Mbunge Dkt Biteko amezidi kuwa kielelezo kikubwa kwa jamii kuwa ni mpenda maendeleo ,jambo ambalo Dkt Biteko amekuwa akilifanya kwa vitendo katika wilaya ya Bukombe.
Aidha amewataka vijana wa Tanzania kuchangamkia fursa za ujuzi zinazopatika VETA ili kuweza kujipatia ujuzi ambao unakwenda kumaliza changamoto zao za ajira.
Pia aliongeza kuwa wananchi wa Bukombe wamekuwa na bahati kubwa kwa kuwa na mwakilishi mwenye kuthamini thamani yao ikiwa tofauti na enzi zetu zilivyokuwa.
MWISHO
0 Comments