MWENYEKITI WA WAZAZI TEMEKE AONGOZA ZOEZI LA UPANDAJI MITI

Na Shushu Joel,Temeke

MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Temeke JIjini Dar es Salaam Ndugu Khamis Slim ameongoza zoezi la upandaji wa miti Zaidi ya elfu moja katika kata ya Chamanzi ili kuweza kusaidia kuongeza uoto wa asili ambao umekuwa ukipotea kutokana na shughuli mbalimbali ambazo zimekuwa zikifanywa na binadamu kila kukicha.

Akizungumza mara baada ya shughuli za upandaji wa miti hiyo Mwenyekiti Slim alisema kuwa wameamua kufanya hivyo ili kuongeza chachu kwa wananchi kuweza kutambua thamani ya uoto wa asili pia kutokomeza maporomoko ya maji jambo ambalo limekuwa likiongeza kila kukicha kutokana na ukatikaji miti ovyo.

 

Aidha aliwataka viongozi wa Chama na serikali kuhakikisha wanaitunza miti hiyo ili iweze kuwa na tija kubwa katika jamii kwani mpaka sasa hakuna mwananchi ambaye hajaona madhara ambayo yamekuwa yanafanywa na maji hasa wale wanaoishi mabondeni na sehemu ambazo zimeathirika na ukataji miti ovyo.

“Niwapongeze sana wananchi wa mtaa wa Mwembe bamia ambao mmejitokeza kwa wingi kushiriki kwenye zoezi la upandaji miti na ni ishara tosha kuwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan anakubalika katika wilaya ya Temeke” Alisema Mwenyekiti Slim

Kwa upande wake Diwani wa kata hiyo John Gama amempongeza Mwenyekiti huyo kwa kuona umuhimu mkubwa na kuwaletea wakazi wa mtaa wa Mwembe Bamia miti hiyo ili kuweza kupandwa kwenye eneo la pembeni mwa barabara.

Aidha aliongeza kuwa ni jukumu letu wananchi kuhakikisha tunaenzi michango mikubwa ya kimaendeleo ambayo inafanywa na viongozi wa chama na serikali  katika kata yetu ya chamanzi.

Diwani huyo aliongeza kuwa miti hiyo inaenda kuwa kielelezo kikubwa kwa wananchi wa chamanzi pia ni vyema nasi kuendeleza kupanda miti hata mitatau kwenye kila kaya zili kuunga mkono juhudi za Mwenyekiti Slim

MWISHO

Post a Comment

0 Comments