Na IRENE TEMU, Katavi
Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko,amewataka wananchi kuchangamkia fursa za kimaendeleo zitakazo kuwepo kuelekea Wiki ya Mwanakatavi inayotarajiwa kuanza Oktoba 25 hadi 31 mwaka huu katika Mkoani aweKatavi.
Akizungumza na Waandishi wa habari,RC Mrindoko amesema maonesho ya Wiki ya Mwanakatavi yatafanyika katika Uwanja wa Azimio uliopo Mjini Mpanda na amewaalika wakazi wote wa Mkoa wa Katavi pamoja na wadau wengine kutoka nchi za Afrika Mashariki na nje ya Afrika kushiriki katika maonesho hayo.
Amesema katika maonesho hayo washiriki watapata fursa ya kujifunza namna ya kuongeza tija katika sekta zote za kiuchumi na kijamii pamoja na kuongeza thamani katika shughuli wanazozifanya pamoja na kuziboresha.
Wiki ya Mwanakatavi mwaka huu itahusisha matukio mbalimbali ikiwepo maonesho ya bidhaa,kujifunza fursa za uwekezaji,fursa katika kilimo,mifugo,uvuvi,utalii sambamba na utamaduni wa Katavi.
Wananchi watapata pia elimu kutoka Taasisi mbalimbali ikiwepo elimu ya upatikanaji wa mikopo,sheria,kanuni na taratibu za makato ya serikali kupitia mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA).
Pia washiriki watajifunza fursa za upatikanaji wa fedha katika shughuli zao wanazozifanya kwa ajili ya kuwainua kiuchumi na kuboresha hali zao za kimaisha.
"katika sekta ya Utalii na Uhifadhi yatafanyika maadhimisho ya miaka 50 ya kuanzishwa kwa Mbuga ya wanyamapori Katavi(Katavi National Park)pamoja na kutangaza vivutio vya utalii katika Mbuga ya Katavi ikiwa ni kuunga mkono jitihada za Mh.Rais Samia Suluhu Hassan katika kutunza utalii wa nchi yetu ya Tanzania"RC Mrindoko.
Hata hivyo RC Mrindoko amesema katika kilele cha wiki ya Mwanakatavi Oktoba 31mwaka huu Serikali ya Mkoa wa Katavi itazindua msimu wa Kilimo kwa mwaka 2024/2025 ambapo itafanyika tathimini ya mahali Mkoa upo katika sekta ya Kilimo kwa mwaka ulioisha 2023/2024 na matarajioa na malengo ya mwaka 2024/2025.
Pia Rc Mrindoko atatangaza mafanikio ya serikali ya awamu ya sita kupitia Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kumshukuru na kumpongeza na kuyatangaza yale yote mema na mafanikio ambayo yamefanyika katika Mkoa wa Katavi katika kipindi chake cha miaka zaidi ya mitatu.
RC Mrindoko ameeleza pia,malengo ya wiki ya Mwanakatavi ni kuhakikisha wananchi wa Mkoa wa Katavi wanajifunza namna ya kuongeza tija katika sekta zote ambazo ni kiuchumi na kijamii pia namna ya kuboresha shughuli wanazozifanya katika Mkoa wa Katavi.
Hivyo ametoa wito kwa wananchi wote wa Mkoa wa Katavi kujitokeza kwa wingi katika maonesho hayo ya Wiki ya Mwanakatavi na kuitumia fursa hiyo vizuri kwa kubadilishana uzoefu kutoka kwa wadau mbalimbali na kutoka na mambo mapya yatakayowasaidia katika shughuli zao za kila siku.
MWISHO
0 Comments