Julieth Ngarabali, Pwani.
Kuweka mahusiano mazuri na uwiano mzuri kati ya kazi na nyumbani ni miongoni mwa mambo yanayopaswa kuzingatiwa kwa wauguzi na wakunga wakati wa kutoa huduma ya afya ya akili kwani tatizo hilo sasa limekua halina tofauti na magonjwa mengine ya mlipuko .
![]() |
| Baadhi ya washiriki wakisikiliza elimu kwa makini |
Hayo yalielezwa juzi na Mhadhiri mwandamizi wa Shule ya Uuguzi na Ukunga ya Chuo Kikuu cha Aga Khan (AKU), Stewart Mbelwa wakati akiwajenge uwezo wahudumu wa sekta hiyo 30 kutoka vituo vya afya mbalimbali vya halmashauri ya wilaya ya Chalinze.
Mafunzo hayo ni mwendelezo wa AKU wa kuwajengea uwezo wauguzi na wakunga na walianzia mkoa wa Dar es Salaam na sasa wamemalizia mkoa wa Pwani katika maeneo ya Kibaha, Mlandizi na Chalinze.
Katika maelezo yake, Mbelwa ambaye ni mtaalam wa sekta hiyo amesema jambo jingine ni wahudumu kujitambua wenyewe kwanza na kuhimili mawazo yao kabla ya kutoa ya kuwahudumia.Alisema hatua hiyo itasaidia kupunguza mlipuko wa magonjwa ya afya ya akili.
" Hawa wataalamu wanapaswa kwanza kuwa na 'stress management' wao wenyewe kabla ya kutoa huduma kwa wateja na wagonjwa wa akili.Hatua hii itasaidia wauguzi na wakunga na kubaini mapema dalili za mtu anayekabiliwa na afya ya akili au wale waliopata mlipuko wa afya ya akili na kuweza kumpa huduma stahiki"alisema Mbelwa.
Katika mafunzo hayo, Mbelwa alisema amewajengea uwezo wauguzi na wakunga namna ya kuwafanyia mazoezi ili wagonjwa ambao wameshaugua afya ya akili ili kurudi katika hali zao za kawaida na kuendelea na shughuli zao za uzalishaji mali.
Baadhi ya washiriki wa warsha hiyo waliishukuru AKU kuwakutanisha pamoja na kuwaongezea elimu wakisema katika mafunzo hayo baadhi ya changamoto zilizokuwa zikitokea kwenye vituo vya afya kati ya wataalamu na wateja mengine yanatokana na upande mmoja kuwa na tatizo la afya ya akili ama kutokujua namna ya kuhuduma mgonjwa wa aina hiyo.
"Tatizo ambalo kwa sasa tumegundua kuwa kabla ya kutoa huduma kwanza kila mmoja akifika eneo lake la kazi ajitathimini kwanza kama hana msongo wa mawazo, au jambo lolote linalomsumbua alilotoka nalo nyumbani au kukutana nalo kazini na ndipo ajue anaweza kuhudumia mteja kweli ama la"alisema Betha Mchopa ambaye pia ni mratibu wa afya ya uzazi na mtoto.
Naye Daudi Gimase alisema jamii inapaswa kuelewa kuwa hata kifafa cha mimba sio matukio ya kishirikina kama inavyojengeka kwenye jamii bali ni ya kitaalamu kwenye ubongo ambapo mjamzito anapokuwa na mambo mengi husababisha kupata ugonjwa wa afya ya akili ama kifafa cha mimba.
" Tunashukuru Aga Khan kutujengea uwezo, wametukumbusha namna ya kuendana na wateja huko vituoni ili kupata huduma stahiki na mtu awe mzima ili aendelee na shughuli zake za uzalishaji kama awali unajua tatizo la afya ya akili inampata mtu ghafla kama ilivyp kwa ugonjwa mwingine wa mlipuko huja na kupotea " alisema Eunice Manyama.
Mwisho


0 Comments