Na Shushu Joel Bagamoyo
"Elimu Bora kwa Maendeleo Bora" ni kauli mbiu inayoibeba taasisi ya Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) iliyopo Bagamoyo Mkoani Pwani iliyojikita katika utoaji Mafunzo ya Uongozi kwa Walimu Nchini. Katika kuhakikisha na kusimamia hilo, Wakala umeendesha
Mratibu wa mafunzo ya uthibiti ubora shule za msingi Bi, Evodia Marco akisoma taarifa ya mafunzo mbele ya mgeni rasmi wakati wa ufungaji wa mafunzo hayo(NA SHUSHU JOEL)
Mafunzo maalum ya Uthibiti Ubora wa
Shule wa ndani kwa Walimu wakuu 284 kutoka Mkoa wa Pwani yaliyofanyika kuanzia
tarehe 13/04/2021 na kufungwa rasmi tar 15/04/2021 na Afisa Elimu Mkoa wa
Pwani, Bi. Hadija Mcheka, katika Kampasi ya Wakala iliyopo Bagamoyo Mkoani
Pwani.
Mafunzo hayo yalijikita katika
kuwajengea uwezo Walimu Wakuu katika maeneo ya
Uthibiti Ubora wa Shule, Ubora wa
Mtaala katika kukidhi mahitaji ya Mwanafunzi, Mafanikio ya Mwanafunzi, Ubora wa
Ujifunzaji na Upimaji mzuri, Ubora wa Utawala ktk Uongozi wa Shule, Ubora wa
mazingira na athari yake katika kuboresha ustawi, Afya na Usalama wa Wanafunzi,
Ufuatiliaji na tathmini ya Uthibiti ubora wa Shule wa ndani.
Afisa Elimu Mkoa wa Pwani Bi. Hadija
Mcheka aliyekuwa Mgeni rasmi katika ufungaji wa mafunzo hayo ameipongeza ADEM
kwa kuratibu na kuendesha mafunzo hayo, yaliyoandaliwa kwa weledi ili kutatua
changamoto za usimamizi wa utoaji huduma bora za elimu katika Shule za Msingi
katika Mkoa wa Pwani.
" Nimefarijika sana kuona Walimu Wakuu wa Mkoa wa Pwani ninaousimamia wamepewa kipaumbele katika kupatiwa mafunzo haya hivyo ni lazima Walimu Wakuu mlioshiriki mafunzo haya mtambue kwamba mna wajibu wa kuhakikisha shughuli ya utoaji wa elimu katika Shule zetu za Msingi, zinatekelezwa kikamilifu na kwa moyo ili watoto wetu waweze kupata elimu bora na si bora elimu" Amesema Bi. Hadija Mcheka.
Baadhi ya walimu wakuu kutoka shule za msingi mbalimbali wilayani Bagamoyo wakifuatilia kwa makini hotuba mbalimbali zilizokuwa zikiytolewa siku ya mwisho ya mafunzo
Akifafanua zaidi Bi. Hadija Mcheka
amesema, nia ya Serikali yetu ni kuendelea kuboresha mazingira ya utoaji wa
elimu katika taasisi za elimu ikiwemo Shule za Msingi kama ilivyofanya katika
kuhakikisha mnapatiwa mafunzo haya.
"Nitumie fursa hii kuwakumbusha
walimu Wakuu wa Mkoa wa Pwani kwenda kuyafanyia kazi maeneo yote ambayo
yamefundishwa katika siku zote tatu za mafunzo, mkatumie vizuri fursa hii ya
mafunzo katika kuimarisha uongozi na ufundishaji katika Shule zetu kwani
kwasasa tunahitaji Uongozi bora unaoleta matokeo chanya na Uongozi unaoacha
alama katika sekta ya Elimu Nchini"
Akimalizia hotuba yake ya ufungaji
mafunzo hayo, Bi Hadija Mcheka, ametoa rai kwa Walimu Wakuu wa Mkoa wa Pwani
waliopatiwa mafunzo hayo kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kutoa
elimu bora, ili kuzalisha wahitimu waliosheheni maarifa na ujuzi, unaowawezesha
kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo na kuahidi kuwa
Mkoa utaendelea kuitumia ADEM katika
mafunzo ya Uongozi na Usimamizi wa elimu na kufanya ufuatiliaji katika Shule za
Msingi kuona kama Walimu Wakuu waliopokea mafunzo haya wanayatumia kuleta
mabadiliko na matokeo chanya katika maeneo yao.
Nae Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa
Maendeleo ya Elimu (ADEM), Dkt. Alphonce Amuli akizungumza katika ufungaji wa
mafunzo hayo, amewashukuru walimu Wakuu 284 kutoka Halmashauri 8 za Mkoa wa
Pwani walioitikia wito wa kuhudhuria mafunzo hayo na kuwataka kuyatumia kama
chachu ya kwenda kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa utolewaji wa elimu bora
katika vituo vyao.
Kwa kipindi kirefu mfumo wa uthibiti
ubora wa Shule wa ndani umekua na changamoto za kiuongozi, zilizopelekea Wizara
ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuona umuhimu wa kufanya maboresho ya mifumo
hiyo kwa kufanya mafunzo haya ya Uthibiti Ubora wa ndani wa Shule kwa Walimu
wakuu, mafunzo yaliyofadhiliwa na mradi wa GPE-LANES II na kuratibiwa na
kuendeshwa na Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM), hii ikiwa ni
awamu ya pili ya utoaji wa mafunzo hayo yaliyotolewa kwa Walimu Wakuu 284
katika Mkoa wa Pwani, 210 kutoka Mkoa wa Songwe na 196 kutoka Mkoa wa Dar Es
Salaama huku awamu ya kwanza ya mafunzo hayo ikiwa imefanyika Mwezi Januari kwa
kutoa mafunzo ya Uthibiti Ubora wa Shule wa ndani kwa Walimu Wakuu wa Shule za
Msingi 8,091 wa Tanzania bara.
MWISHO
0 Comments