Na Shushu Joel
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imefanya uamuzi wa kujenga Vyuo vya Ufundi Stadi nchini ili wananchi hususani vijana wapate ujuzi na ufundi wa aina mbalimbali utakaowawezesha kujiajiri na kuajiriwa.
Ametoa kauli hiyo leo (Jumatatu, Novemba 29, 2021) baada ya kukagua na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa chuo cha ufundi stadi cha wilaya ya Chunya mkoani Mbeya. Ameagiza ujenzi huo ukamilike kwa wakati ili malengo ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata elimu ya ufundi chuoni hapo yanafikiwa.
Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali imeamua kujenga vyuo hivyo vya ufundi stadi ili kufungua milango ya ajira kwa kuwa mafunzo yanayotolewa yatawawezesha wahusika kujiariwa kutika sekta mbalimbali ikiwemo ya viwanda. “Ninawaomba wananchi muendelee kuwa na imani na Serikali yenu.”
Kadhalika, Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa mkoa wa Mbeya uhakikishe katika eneo hilo la kijiji cha Mbugani kinapojengwa chuo hicho kunakuwa na huduma zote za kijamii zitakazotosheleza matumizi ya eneo hilo zikiwemo za maji safi na salama na umeme.
Pia, Mheshimiwa Majaliwa amesema Mheshimiwa Rais Samia anawasihi wananchi waendelee kuyalinda maeneo yao yaendelee kuwa tulivu ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo. “Suala la kuimarisha ulinzi na usalama ni jukumu la wananchi wote, hivyo tuendelee kushirikiana katika kuimarisha ulinzi.”
0 Comments