ONGEZENI THAMANI KWA WANAWAKE " DKT. BITEKO

Na Shushu Joel ,Bukombe.

MBUNGE wa Jimbo la Bukombe Mkoani Geita Dkt. Doto Biteko amewataka wanaume kuongeza thamani kwa wanawake ambao wamekuwa nguzo imara ya maendeleo katika taifa 

Mwanamke ni nguzo duniani kutokana na uimara wake katika  masuala mbalimbali katika jamii na hasa ya kupambana na malezi jambo ambalo kina baba wengi limewashinda kutokana na majukumu yao ya kila siku.

Akizungumza katika Viwanja vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ,Kata ya Igulwa Wilayani Bukombe katika sherehe za maadhimisho ya siku ya wanawake Dkt. Biteko amesema  kuwa popote pale kwenye  maendeleo lazima ukute mwanamke shupavu nyuma.

Amesema kuwa maadhimisho ya siku ya wanawake Wilaya ya Bukombe iwe chachu kubwa katika  kuleta maendeleo kwa serikali kutokana na jinsi ambavyo Mungu kawapendelea hivyo nawasisitiza  mzidi kumsaidia kimawazo na kiutendaji Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ameonesha uongozi thabiti katika taifa na hata kuweza kutunukiwa medali mbalimbali ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

"Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan katuletea mikopo nafuu inayopatikana kwenye Halmashauri yetu hivyo ni vyema kila mmoja akachangamkia fursa hizo kwani lengo la mikopo hiyo ni kuwaondoa katika lindi la umasikini na kukuza uchumi wao" amesema  Dkt. Biteko. 

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya hiyo Mhandisi  Paskasi Muragili amempongeza Mbunge wa Jimbo hilo kwa ushauri wake kwa wanawake wa Bukombe juu ya kuongeza ubunifu wa malezi kwa familia zao.

Aidha amewakumbusha wanawake kuendelea kuwa shupavu katika kusukuma gurudumu la maendeleo na  kuzidi kuwa wabunifu katika shughuli zenu mbalimbali ili muweze kujikwamua na kukwamua familia kwa ujumla.

DC Muragili amemuomba Mhe Mbunge Dkt Biteko kupeleka salamu za wanawake wa Wilaya ya Bukombe kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa wanampenda na wataendelea kumsemea kwa jinsi ambavyo amewaheshimisha katika masuala mbalimbali. 

Naye Jazaa Komba amewapongeza wanawake wenzake kwa kujitokeza kwa wingi siku  kwenye sherehe hiyo jambo ambalo linaonyesha kuwa wanawake tunaweza hata tusipowezeshwa.

"Kila mwanamke akimuona Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan mambo makubwa anayoyafanya basi huzidisha ari  ya kufanya kazi huku  kila mmoja wetu" amesema  Mwl. Jazaa Komba.

MWISHO

Post a Comment

0 Comments