DIWANI UBENA AMALIZA MIGOGORO YA ARDHI KWA 90%

Na Shushu Joel,Chalinze.

DIWANI wa kata ya Ubena halmashauri ya Chalinze wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani Gofrey Kamugisha kwa kushirikiana na baraza la Ardhi la kata hiyo wamefanikiwa kutataua changamoto mbalimbali za migogoro ya Ardhi baina ya mtu na mtu na ile ya mashamba makubwa ya wakulima na wafugaji kwa Asilimia 90.

Diwani wa kata ya Ubena Mhe Kamugisha akifuatilia jambo

Akizungumza katika uwasilishaji wa utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) ya kata hiyo  kwa kipindi cha miezi sita sasa Diwani huyo alisema kuwa kipindi cha nyuma migogoro ilikuwa ni mingi na wengi walikuwa wakigombea mipaka midogo midogo ambayo imekuwa ikiwasumbua wananchi wa kata hiyo.

“Migogoro ya Ardhi imekuwa ikichangia kwa asilimia kubwa sana kwa wananchi mbalimbali kutokuelewana na hata kupelekea ugomvi mkubwa kitu ambacho kimekuwa kikirudisha maendeleo ya kata yetu nyuma hivyo tumeamua kupambana nayo ili kuondoa na tuweze kusonga mbele kimaendeleo” Alisema Kamugisha

Aidha aliongeza kuwa panapokuwa na migogoro ya Ardhi katika eneo lolote lile maendeleo ni magumu sana kwa jamii hivyo kwa kuwa tumefanikiwa kama kata kutatua changamoto hizo kwa kiasi kikubwa kwani tumemaliza kesi 180 na 2 tu tumepeleka kwenye baraza la Ardhi wilaya hivyo hii ni hatua kubwa katika maendeleo.

Naye Mwidini Ally amempongeza Diwani huyo kwa utendaji wake wa kazi kwa wananchi wa Ubena kwani maendeleo yalikuwa nyuma lakini tangu Kamugisha kuchukua kijiti cha uongozi kumekuwa na mabadiliko makubwa katika sekta ya mbalimbali za maendeleo.

Kwa upande wake mgeni rasmi wa mkutano huo ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Bagamoyo Sharifu Zahoro amempongeza Diwani huyo kwa utekelezaji wa Ilani ndani ya miezi sita.

Hivyo amewataka madiwani wengine kuiga mfano huo ulionyeshwa na Diwani wa Ubena kwa kuwasaidia wananchi kwa asilimia kubwa na hii ndio CCM tunayohitaka kwa wananchi wetu. Aidha Mwenyekiti huyo aliongeza atakuwa mkali kwa viongozi wote wanaotokana na CCM kwa kutokuwasaidia wananchi wao kwa yale tuliyoyaahidi kwao kipindi cha kampeni.

MWISHO

 

Post a Comment

0 Comments