KISARAWE WALILIA MBOLEA

 Na Shushu Joel, Kisarawe.

MADIWANI wa halmashauri ya wilaya ya Kisarawe Mkoani Pwani wameiomba serikali kupitia wizara ya kilimo kuharakisha zoezi la usambazaji wa mbolea katika wilaya hiyo kwani baadhi ya  wakulima tayari wamekwisha anza kulima bila mbolea.

Mwenyekiti wa halmashauri ya Kisarawe Zuberi Kizwezwe akizungumza na madiwani(NA SHUSHU )

Kilio hicho kimetolewa katika kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo.na mmoja wa madiwani ambapo alidai sasa mvua zimeanza kunyesha lakini wakulima hawana mbolea


Akitoa hoja hiyo diwani wa kata ya Maneromango  Hamisi Dikupatile alisema kuwa wakulima wamesha  andaa mashamba lakini cha ajabu mpaka sasa mbolea bado ni changamoto.


Aliongeza kuwa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kupitia waziri Bashe imekwisha toa mwongozo wa jinsi gani wakulima wanavyoweza kupatiwa mbolea lakini kisarawe bado mambo hayajaeleweka kwa wakulima wetu.


"Mpaka sasa baadhi ya wakulima wamekwisha anza kupanda mazao kama mahindi na mengine hivyo kucheleweshwa kwa mbolea kwa wakulima ndio chanzo cha kutokupata kwa mavuno mengi kwa wakulima wetu" Alisema Dikupatile


Naye Diwani wa viti maalum Tarafa ya Maneromango Mhe  Badria Hassan alisema kuwa ni vyema wataalam wetu wa idara ya kilimo,Mifugo na Uvuvi wakajikita zaidi kuelimisha wakulima juu ya umuhimu wa uwekaji wa mbolea mashambani hivyo elimu hii ikiwafikia kwa haraka itasaidia kuwainua wakulima kupitia nyanja ya kilimo.


Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya  kisarawe James Chitumbi alisema kuwa serikali kupitia wizara ya kilimo, Mifugo na Uvuvi tayari imekwisha leta baadhi ya majina hivyo kilichobaki mpaka sasa ni kuwatembelea wakulima na kuwapatia elimu .


Aidha Chitumbi amewatoa hofu madiwani juu ya mbolea kwani kila jambo linaenda vizuri na litatekelezeka kwa wakati kama lilivyopangwa na serikali kupitia wizara. 


MWISHO.

Post a Comment

0 Comments