Na Shushu Joel
Serikali imemega baadhi ya maeneo ya Ranchi ya Kagoma yenye ukubwa wa
hekta 50,690 na kuyarasimisha kwa wananchi wa Kata ya Rutoro wilayani
Muleba mkoani Kagera ili kwa ajili ya shughuli za makazi, kilimo na ufugaji .
Kauli hiyo imetolewa na Kamati ya Mawaziri wa Kisekta katika mkutano
wa hadhara uliofanyika katika eneo la Shule ya Msingi Rutoro, Muleba .
Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia ni
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) amesema maeneo
hayo yatamegwa na kupewa wananchi kwa kuzingatia ushauri wa watalaam.
“Maeneo yatakayomegwa kwa kuzingatia ushauri wa wataalamu kutoka
kwenye ranchi yatawekewa utaratibu wa usimamizi na uongozi wa mkoa
ukishirikiana na wilaya ili msigombanie au kufanya jambo lolote ndani ya
maeneo hayo” Mhe. Ndaki amesisitiza.
Mhe. Ndaki amewaonya viongozi wa vijiji na vitongoji kuacha tabia ya kugawa
maeneo hayo kwa kuwa hawana mamlaka ya kugawa maeneo.
Katika hatua nyingine, amesema Serikali imeridhia kukiacha Kitongoji cha
Rwamisha B ambacho kiko wilaya ya Karagwe chenye kaya 480 ambacho
awali kiliamuliwa kiondoke.
Mhe. Ndaki ameelekeza mkoa wa Kagera kuandaa mpango wa utekelezaji
wa maamuzi ya Kamati ya Mawaziri ya Kisekta yaliyofikiwa ikiwa ni pamoja
na kurekebisha mipaka ya vijiji kwa kuzingatia maoni ya wataalamu.
Sambamba na hilo Waziri Ndaki amewatoa hofu wawekezaji walioko katika
Ranchi ya Kagoma akiwaeleza kuwa wako salama na Serikali imefanya
mazungumzo na Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) ili uwekwe utaratibu
mzuri ambao utawawezesha kupewa maeneo yatakayomegwa.
Amewaasa wananchi kuwa watulivu wakati wa utekelezaji wa maamuzi ya
kamati hiyo na kuacha kuvamia maeneo ili kurahisisha utekelezaji wa
maamuzi hayo.
Naye, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe.
Ridhiwani Kikwete (Mb) amewataka wananchi kuendelea kuheshimu sheria
za ardhi hususani katika mpango wa maendeleo ya ardhi na kwamba kuna
kazi ya kufanya katika kuhakikisha miundombinu na majengo ya eneo la
Rutoro yanakaa sawa.
Ametoa rai wananchi hao kuwa watulivu mpaka wataalamu wa ardhi
watakapokuja kutoa utaratibu wa maeneo yaliyoachiwa kwa wananchi.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja
(Mb) amewataka wananchi wa Kata ya Rutoro kuitumia ardhi waliyoachiwa
kwa maendeleo kwa kuanzisha miradi ya upandaji miti pamoja na ufugaji
nyuki.
“Nendeni mkapande miti kibiashara mtapata mbao na wakati huohuo
mnaweza kuanzisha miradi ya ufugaji nyuki.
Ametoa wito kwa wananchi kutoyavamia maeneo yatakayoachwa kwa
Serikali kwa kuwa ni maeneo yanayotunzwa kwa faida ya kizazi cha leo na
kinachokuja.
Kamati ya Mawaziri wa Kisekta imehitimisha ziara yake mkoani Kagera na
itaendelea na zoezi hilo katika mkoa wa Ruvuma.
MWISHO



0 Comments