UKATILI UNADUMAZA WANAWAKE KIUCHUMI: SUBIRA MGALU

Na Shushu Joel,Bagamoyo

MBUNGE wa viti maalum kupitia Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mkoa wa Pwani Subira Mgalu amesema kuwa vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa watoto na wanawake vinazidi kuongezeka nchini na hivyo kupelekea wanawake walio wengi kudumaa kiuchumi 

Mbunge wa viti maalu Mkoa wa Pwani Subira Mgalu akifafanua jambo mbele ya wanawake wa kata ya Fukayosi (NA SHUSHU JOEL)

Mgalu alisema hayo hivi karibuni wakati alipokuwa akiongea na wanawake wa kata ya Fukayosi iliyoko wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani kwenye uzinduzi wa mradi wa maji safi na salama ulijengwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan.

Alisema kuwa takwimu za mwaka 2021 zinaonyesha kuwa Zaidi ya watoto asilimia 15% wamefanyiwa ukatili hivyo hali hii inapelekea kudumaza uchumi wa wanawake kutokana na wengi wao kujikita kupambania afya za watoto wao na kuacha kuendesha shughuli zao za uchumi.

Aidha aliongeza kuwa kutokana na kuongezeka kwa matukio hayo ya kikatili kuongezeka nchini, Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dtk Samia Suluhu Hassan imeamua kulivalia njuga jambo hili na kuamua kuja na mikakati ya uwezeshaji kiuchumi makundi hayo kwa lengo la kuwa na biashara za kufanya.

Mbali na hilo Mgalu amewataka wanawake kuendelea kuunda vikundi mbalimbali ambavyo vitaweza kukopesheka kwa urahisi kwenye halmashauri zetu mbalimbali.

“Nitawaletea wataalamu mbalimbali kutoka benki ili waje wawapatie elimu juu ya uendeshaji wa biashara” Alisema Subira Mgalu


Kwa upande wake Diwani wa kata hiyo Ally Ally amempongeza Mbunge wa viti maalum Subira Mgalu kwa jinsi ambavyo amekuwa msaada kwa wanawake wa Mkoa wa Pwani katika masuala mbalimbali na hasa ya upingaji ukatili na lile la kuwasaidia kukuza uchumi wao kimakundi na binafsi.

Aidha amemtaka aweze kuendelea na moyo huo wa kujitoa kwa jamii hivyo inaonyesha kuwa ni jinsi gani Mgalu alivyo msaidizi sahihi kwa Rais wetu Dkt Samia Suluhu Hassan.

Naye Bi, Aisha Muhamed amempongeza Mbunge Subira Mgalu kwa jinsi ambavyo amekuwa akiwapambania katika kupinga ukatili na kukuza uchumi wao,

MWISHO

Post a Comment

0 Comments