MALAWI WATUA ILEJE KUJIFUNZA HIFADHI YA MAZINGIRA

NA MWANDISHI WETU ILEJE

Mkuu wa Wilaya ya Chitipa kutoka nchini Malawi Mhe.McMillan Magomero ameongoza timu ya watalaam wa utekelezaji wa Mradi wa Hifadhi ya Bonde la Mto Songwe kutembelea Wilaya ya Ileje mkoani Songwe kwa lengo la kujifunza  uhifadhi wa mazingira.

Mkuu wa Wilaya ya Ileje Farida Mgomi akiteta jambo na mgeni wake ambaye ni Mkuu wa Wilaya kutokea nchini Malawi

Ugeni huo umeshiriki kikao leo Alhamisi Machi 24,2023 pamoja na timu kama hiyo kutoka Wilaya ya Ileje ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya Mhe.Farida Mgomi.


Akifungua kikao hicho cha siku moja kinachoendelea kwenye Ukumbi wa VIM uliopo Itumba Mhe.Mgomi amesema kuwa ziara hiyo ni muhimu kwa pande zote mbili kwa vile kila upande unahitaji kujifunza.


Naye Mkuu wa Wilaya ya Chitipa amesema kuwa kufanyika kwa ziara hiyo ni mwendelezo wa kuimarisha mahusiano ya kindugu yaliyojengwa  hata kabla ya ujio wa wakoloni.


Hapo kesho Ijumaa timu hizo zinatarajia kutembelea vijiji vya Bulanga,Ilondo na Malangali vilivyopo katika Kata ya Malangali Tanzania ili kukutana na wananchi na kuona jinsi wanavyoshirikishwa katika miradi ya awali ya hifadhi ya mazingira inayohusiana na Mradi wa Hifadhi ya Bonde la Mto Songwe ambao ni mpaka wa nchi hizi mbili ukiwa na tabia ya kuhamahama wakati wa masika hususani wilayani Kyela inakopakana na Wilaya ya Karonga.


Taarifa za kikao hicho zimeeleza kuwa katika kata ya Malangali watakakotembelea hapo kesho kuna miradi ya kilimo cha kahawa na parachichi ambayo ipo pia  Malawi katika vijiji vya Njebete 1,Njebete 2 na Njebete 3.


Mradi wa Uhifadhi wa Bonde la Mto Songwe unahusisha Wilaya za Kyela,Ileje,Mbozi,Momba na Mbeya Vijijini upande wa Tanzania huku Wilaya za Chitipa na Karonga upande wa Malawi zikihusika.

MWISHO

Post a Comment

0 Comments