Julieth Ngarabali,, Mkuranga.
Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga ya mkoani Pwani Khadija Ally amepiga marufuku watoto wa umri wa miaka chini ya mitano na Wanafunzi wa shule za msingi kuingia kwenye vibanda vya kuangalia video maarufu vibanda umiza ikiwa ni moja ya mikakati ya kuwalinda na vitendo vya ukatili wa kijinsia, ulawiti na ubakaji.
![]() |
Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Khadija Ally |
Amesema hayo wakati akizungumza na Mwandishi wa habari hizi huko Mkuranga ambapo amesema wapo watoto wadogo kuanzia miaka miwili kuendelea wamekuwa wakionekana kwenye vibanda hivyo huku wazazi na walezi wakiwa hawana habari nao jambo ambalo sasa halikubaliki na wahusika watawajibishwa.
Amesema Wilaya sasa imeweka nguvu kubwa katika kupambana na hali hiyo ili kumaliza vitendo vya ukatili wa kijinsia, ubakaji na ulawiti kwa watoto wilayani humo ambapo mtoto, mzazi na mmiliki wa vibanda vya sinema watamchukuliwa hatua kali za kisheria.
"katika kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia, ulawiti na ubakaji kwa watoto uongozi wa Wilaya kwa kushirikiana na Kamati ya ulinzi na usalama na Jeshi la Polisi wamekubaliana kutofumbia macho wazazi na walezi ambao hawana nia njema na watoto wa Mkuranga na taifa kwa ujumla."amesema Mkuu huyo
Akielezea takwimu za matukio ya ukatili na hatua zilizochukuliwa amesema tayari watu watatu waliobainika kubaka wamefikishwa mahakamani na wawili kati yao wamekwishahukumiwa miaka 30 jela kwa kosa la ubakaji.
"Tunashukuru haki imetendeka wamekwisha hukumiwa wawili kati yao na nitoe rai kwa Wananchi kwamba vyombo vya usalama hatutaweza kuendelea kufumbia macho Wananchi wasiona nia njema na watoto wetu" alisema Khadija.
Aidha amewashukuru Wananchi wa Wilaya hiyo wanaoendelea kutoa taarifa za kuwafichua wanaojihusisha na vitendo hivyo vya ukatili wa kijinsia, ulawiti na ubakaji kwa watoto kwenye vyombo vya usalama na vyombo vya sheria ili hatua kali zichukuliwe dhidi ya waharifu hao na hatua kali za kisheria haraka huchuliwa dhidi ya waharifu hao.
"Tutaendelea kuchukuwa hatua Kali dhidi ya wahalifu hao ili iwefunzo kwa wengine kwa lengo la watoto na Wananchi wa Wilaya ya Mkuranga wawe salama" amesema.
Aidha Mkuu huyo wa Wilaya ya Mkuranga amesema tayari wameanza kuelimisha Wazazi na Wanafunzi katika shule 38 kati yake shule 18 ni za msingi namna ya kujilinda na ukatili wa kijinsia kwa kushirikiana na Dawati la jinsia la Jeshi la Polisi, idara ya Maendeleo ya Jamii na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo.
Akizungumzia watoto kuzurura mitaani wakati wa jioni na usiku Khadija amesema Wazazi watawajibika kwa watoto wao kuzurula bila uangalizi muda wa jioni na usiku kwa mujibu wa sheria za nchi kwani ni lazima mzazi ajue ratiba ya mtoto kwani bado yupo chini ya uangalizi wao.
Mmoja wa wazazi Furaha Eliamani amepongeza hatua hiyo na kusema ikitekeleawa ipasavyo itasaidia kupunguza idadi ya watoto wanaozurura hovyo mitaani muda wa zaidi ya saa 12 kwani sheria zinazomlinda Mtoto zipo wazi 'hili lazima Wazazi wenzangu tukubaliane "
Hata hivyo mkazi wa Mtaa wa Mwandege Fadhili Abdul amesema wengi wa watoto wanapenda kwenye vibada vya video ni wale wanaoishi mazingira magumu ambapo baadhi huishi na bibi na Babu baada ya wazazi kuwatelekeza ama kufariki na kadhaa ni wale ambao wazazi wao wanakua wazembe tu kwenye malezi.
Takwimu za matukio ya ukatili kwa watoto katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2021 iliyotolewa na Jeshi la Polisi nchini mapema mwaka 2023 ni kwamba matukio yaliyoripotiwa ndani ya Jeshi hilo ni 11,499 ikilinganishwa na matukio 15,870 katika kipindi kama hicho mwaka 2020, sawa na upungufu wa matukio 4,371 ikiwa na asilimia 27.5.
Mwisho.
0 Comments