Julieth Ngarabali,, Kibaha..
Wananchi katika kitongoji cha Disunyara kata ya Kilangalanga Wilayani Kibaha wameanzisha utaratibu wa watoto wenye umri wa miaka miwili mpaka mitano kulelewa kwenye vituo maalumu vya kijamii vya makuzi na malezi ya watoto (day care) ili kwanza kuwaepusha na.matukio ya ukatili na pia wazazi waweze kwenda kujishughulisha na shughuli za ujasiriamali na kujiingizia kipato
Wakizungumza kwenye mapokezi ya vifaa mbalimbali vya kujifunzia, kuchezea, usafi, na kupikia vilivyotolewa na Taasisi ya Anjita Child Development Foundation wamesema wamefikia hatua hiyo baada ya kujua faida ya vituo hivyo ni pamoja na yanamsaidia mtoto kuchangamka kiakili ukilinganisha na watoto wanaolelewa nyumbani na kuepuka matukio ya ukatili na unyanyasaji.
Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia ,Wanawake na Makundi katika kipindi cha January hadi Desemba mwaka 2022 jumla ya matukio ya ukatili kwa watoto yalikua ni 12,163 wavulana 2,201 na wasichana 9,962 ikilinganishwa na matukio 11, 499 kwa mwaka 2021 sawa na ongezeko la asilimia 5.8.
Mwenyekiti wa kitongoji hicho Tatu Jalala.amesema wao kama jamii katika kuona umuhimu wa vituo vya malezi kama hicho wameamua kuchangia marekebisho ya vyoo, jiko, kuhamasisha wazazi na kuratibu usimamizi wa kituo hicho
Katibu wa kituo na mzazi Imelda Justus ameongeza kuwa wameshaanza kuandikisha watoto ambapo tayari watoto 25 wameshaandikishwa na wataanza kulelewa hapo kuanzia Julai 20 mwaka huu na kwamba kituo ni cha kijamii kutakua kinaendeshwa na Wananchi chini ya usimamizi wa idara ya ustawi na maendeleo ya jamii.
Imelda amesema utaratibu wa kumpata Mwalimu wa kituo hicho cha malezi na makuzi umefuata taratibu zote ikiwemo ya kutangaza nafasi hiyo na maombi yote kupitiwa na hivyo wanaamini mlezi huyo atawalea watoto kwa uadilifu na upendo na sio kuwa mkatili.
Awali akikabidhi vifaa hivyo, mkurugenzi wa Anjita Janeth Malela amesema kwa kushirikiana na Serikali ya Halmashauri ya Kibaha wameuhisha kiituo hicho cha kijamii baada ya uongozi wa Kitongoji kuiomba taasisi ya Anjita kuhuisha na kusaidia katika usimamizi , kuwajengea uwezo wanakamati na walezi ili kituo kiweze kufanya kazi baada ya kusimama kwa takribani mwaka mmoja.
"Hvyo Anjita kwa kushirikiana na serikali ilichukua hilo jukumu kwa kutekeleza kazi mbalimbali za uhuishaji wa kituo hko ikiwepo kufanya mikutano na viongozi wa serikali, wazazi/ walezi, kamati mpya iliyoundwa, kufanya tathmini ya mahitaji ili kituo kifunguliwe upya. siku ya leo tumekabidhi vifaa hivyo kama mchango wetu kwa Kituo" amesema Malela
Faida ya vituo vya makuzi na malezi ya awali ya watoto ni pamoja na kumsaidia mtoto kuchangamka kiakili ukilinganisha na watoto wanaolelewa nyumbani ambapo kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa katika nchi zilizoendelea zinathibitisha kuwa watoto waliopelekwa kwenye vituo vya malezi mapema wanakuwa wachangamfu kiakili kuliko wenzao wanaolelewa nyumbani.
Pia sababu kubwa ni kuwa katika kituo mtoto anakuwa na fursa ya kuchangamana na wenzake wanaotoka kwenye familia nyingine, kucheza, kuzungumza, kuwasiliana na wenzake humfanya ajifunze mambo mapya kwa wepesi kuliko kama angekuwa mwenyewe nyumbani.
Mwisho
0 Comments