Na Shushu Joel, Bukombe
MBUNGE wa Jimbo la Bukombe na Waziri wa Nishati ambaye pia ni Naibu Waziri Mkuu Mhe Dkt Dotto Biteko amewataka watanzania kutokubaguana kwa ajili ya dini,makabila na hata vyama vya kisiasa.
![]() |
Naibu Waziri Mkuu Dkt Biteko akisisitiza jambo kwa wananchi wa Jimbo la Bukombe waliofurika kujitokeza kwenye mikutano aliyofanya ( NA SHUSHU JOEL) |
Rai hiyo ameitoa alipokuwa akizungumza na Wananchi wa kata ya Namonge katika jimbo lake la Bukombe Mkoani Geita.
Dkt Biteko alisema kuwa waasisi wa Taifa letu walipinga vikali masuala ya ubaguzi wa aina yeyote ile hivyo ni wakati wetu kuyaenzi kwa vitendo yale yote ambayo waasisi wetu walituachia watoto wao.
" endapo tukianza kubagua itatutenganisha kutokana na kuwa sisi sote sio kabila moja, dini moja na wala sio wote ni wana Chama Cha Mapinduzi (CCM) hivyo ni wakati sasa wa kuendeleza umoja wetu" Alisema Naibu Waziri Mkuu Dkt Biteko
Aidha amewakumbusha wananchi wa kata hiyo ya Namonge kukumbuka walikotoka na walipo sasa katika sekta ya maendeleo kwani tulikuwa nyuma sana kwenye nyanja mbalimbali za kimaendeleo.
Pia amewataka wananchi wa Bukombe na watanzania kwa ujumla kuzidisha maombi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt Samia Suluhu Hassan kwani tangu aongoze nchi imefanikiwa kupiga hatua kubwa kwenye maendeleo na hata nyie Bukombe mnamuona Rais wetu anachotufanyia
Kwa upande wake Diwani wa Namonge Ndg, Mlalu Bundara akizungumza kwa niaba ya Wananchi hao alisema kuwa Dkt Biteko amekuwa nguzo kubwa ya maendeleo ya kata yetu kwani kila sekta Namonge imekamilika .
Aidha amewataka wananchi kuandaa zawadi ya kumpa Naibu Waziri Mkuu ili aendelee kututumikia na zawadi hiyo si kubwa bali kumpatia viongozi wanaotokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM) .
MWISHO
0 Comments