TANZANIA KUPATA NEEMA KUTOKA SHIRIKA LA UTALII LA UMOJA WA MATAIFA LA (UNWTO), NI LA KUTANGAZA UTALII WA TANZANIA

NA MWANDISHI WETU,

 CAPE VERDE.

SHIRIKA la Umoja wa Mataifa la Utalii (UNWTO) limeahidi kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuweka mikakati bora ya kuwajengea uwezo  watu waliopo katika sekta ya utalii.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro akimuonesha  baadhi ya vivutio vya utalii vilivyopo katika jarida la Utalii kutoka Tanzania Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Kimataifa linaloshughulikia Masuala ya Utalii (UNWTO) Zurab Pololikashvili (kushoto)  mara baada  kufanya kikao cha ana kwa ana kando ya mkutano huo wa  Kimataifa wa Utalii wa Kanda ya Afrika unaofanyika kwa muda wa siku nne kuanzia jana  tarehe 2 Septemba  hadi 6 mwaka huu  katika Kisiwa cha SAL nchini Cape Verde

Hatua hiyo inakuja kufuatia hali mbaya inayoikumba sekta ya Utalii nchini na Duniani kwa ujumla kufuatia janga la virusi vya UVIKO 19.

Ambapo pia ikikadiriwa kuwa, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imepata hasara ya Dola 4.8 bilioni za Marekani (Zaidi ya Sh Tirioni 11) kwenye sekta ya utalii kutokana na janga hilo la  UVIKO 19 huku watu milioni 21 wakikosa ajira.

Akizungumza na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro, Katibu Mkuu wa UNWTO, Zurab Pololkashvili amesema mafunzo hayo yatakayotolewa kwa Wadau wa Utalii yatalenga kuwajengea uwezo Wadau hao katika kujiimarisha na kuendana na janga la UVIKO 19 katika kuendesha shughuli za utalii nchini.


Amesema mafunzo hayo pia yatawalenga watu mbalimbali wenye nia ya kutaka kuingia katika sekta ya utalii nchini ilikutengeneza ajira nyingi kupitia utalii.


Ujumbe wa Tanzania unahudhuria mkutano huo ulioandaliwa na Shirika la UNWTO wa 64 wa Kanda ya Africa ukiongozwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro unaofanyika kwa muda wa siku nne  katika Kisiwa cha Sal kilichopo  nchini Cape Verde.


Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu huyo amemueleza Waziri Dkt. Ndumbaro kuwa UNWTO  iko mbioni kuandaa Kalenda  ya mwaka ya UNWTO  ambapo Tanzania nayo itakuwemo katika orodha hiyo kuendana na matukio yatakavyopangwa katika mkutano huo.

"Moja ya kipaumbele cha UNWTO kwa sasa ni kuitangaza Tanzania na Africa kwa ujumla.Hii pia ni pamoja na kujengea uwezo wadau wa Utalii katika kujiimarisha na kuendana na jangaa UVIKO 19 katika kuendesha shughuli za Utalii Tanzania". Alisema Katibu  Mkuu huyo wa UNWTO, Bw. Zurabu Pololkashvili. 

Kwa upande wake, Waziri Dkt. Ndumbaro akizungumza katika kikao hicho cha ana kwa ana na Katibu Mkuu huyo, amesema mafunzo hayo yatatoa matumaini kwa Wadau wa Utalii nchini baada ya ugonjwa wa UVIKO 19 kuwatikisa.

Katika hatua nyingine Waziri, Dkt. Ndumbaro amemueleza Katibu Mkuu huyo kuwa Tanzania ni nchi ya kwanza Afrika kwa shughuli za Uhifadhi ila katika suala la kujitangaza na kutafuta masoko bado kuna changamoto hivyo ujio wa mafunzo hayo yatawezesha Serikali na Wadau wa Utalii kujiimarisha katika nyanja hiyo.

Aidha, Dkt. Ndumbaro amemualika Katibu Mkuu huo wa UNWTO, kuja kutembelea vivutio vilivyopo Tanzania na kusisitiza kuwa ataambatana naye katika ziara hiyo ya kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo nchini.

Mwisho

Post a Comment

0 Comments