Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Shimbale iliyoko halmashauri ya mji wa Bariadi mkoani Simiyu anashikiliwa na jeshi la Polisi mkoani hapo kwa tuhuma za kufanya udanganyifu kwenye mtihani wa darasa la nne uliofanyika Oktoba 28 na 29 mwaka huu.
Kamanda wa jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu Kamishina Msaidizi Shadrack Masiji |
Akizungumza na waandishi wa habari, kaimu kamanda wa jeshi la polisi mkoani hapo kamshina msaidizi wa jeshi la polisi Shadrack Masiji amesema mwalimu huyo alifanya udanganyifu kwenye mitihani ya darasa la nne kwa kuwachukua wanafunzi wa darasa la tano na la sita kwaajili ya kuwafanyia mtihani wanafunzi wa darasa la nne ambao ni watoro.
Masiji amemtaja mwalimu mkuu huyo kuwa ni Gaudensia Onyango (45) mkazi wa mtaa wa shimbale kwa tuhuma za kufanya udanganyifu huku akifafanua kuwa wanafunzi wa darasa la nne hutumia kadi za maendeleo kwa ajili ya usajili na ukaguzi wakati wa mitihani, hivyo mwalimu huyo alikuwa akitoa picha za wanafunzi watoro na kuweka picha za wanafunzi wa madarasa ya juu ili waweze kufaulu.
"serikali kupitia wizara ya elimu kwa kushirikiana na TAMISEMI wamekuwa wakitoa zawadi kwa shule zinazofanya vizuri, hivyo lengo la mwalimu huyo lilikuwa ni shule yake kupata ufaulu mzuri ili waweze kupata zawadi na kuwa kwenye nafasi nzuri kimatokeo" amesema Masiji huku akiongeza kuwa:
" hadi sasa mtuhumiwa yupo mahabusu na anaendelea kuhojiwa kuhusiana na tuhuma hizo, na mara baada ya upelelezi kukamilika jalada litafikishwa ofisi ya taifa ya takwimu kwa mashtaka na hatua za kisheria ikiwemo kufikishwa mahakamani zitafuata " Masiji
Aidha Masiji amewataka watumishi wote wanaohusika na zoezi la usimamizi wa mitihani wa kidato cha pili na kidato cha nne kuacha mara moja vitendo vyovyote vya udanganyifu wa mithani kwani kamati za mithani ya wilaya na mkoa kwa kushirikiana na jeshi la polisi halitafumbia macho suala ya udanganyifu katika mitihani hiyo.
Na Anita Balingilaki ,Bariadi.
0 Comments