Na Shushu Joel
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb)ameitaka
menejimenti Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA)
ifanye kazi kwa ushirikiano ili kuiwezesha taasisi hiyo kutimiza malengo
yaliyowekwa.
Mhe. Mary Masanja ametoa kauli hiyo leo jijini Mwanza mara baada ya
kuitembelea menejimenti ya TAWA inayoendelea na mafunzo ya uongozi
katika Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Pasiansi.
Amewaeleza kuwa utendaji kazi wenye kuzingatia ushirikiano na Upendo ni
nguzo muhimu itakayowawezesha kurekebishana na kukosoana kiutendaji
kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.
Aidha, amesisitiza kuwa ni vyema menejimenti hiyo ikajiwekea utaratibu wa
kujadili changamoto mbalimbali pamoja ili iweze kufika mbali kiutendaji.
"Mwenzako anapokutana na changamoto yoyote ichukulie kama ni yako.
Tunahitaji tufanikiwe kwa kutatua changamoto zinazotukabili kwa pamoja "
amesisitiza Mhe. Masanja.
Mafunzo hayo yenye lengo la kuwajengea uwezo viongozi katika usimamizi
wa masuala mbalimbali yakiwemo ya rasilimali watu, fedha na taratibu za
manunuzi yametolewa kwa Manaibu Kamishna, Makamanda wa Kanda,
Makamishna Wasaidizi Wandamizi na Makamishna Wasaidizi.
0 Comments