NA SHUSHU JOEL
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mwanza, ambaye pia ni Naibu Waziri wa
Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja akiwa ameambatana na Umoja wa
Wanawake wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Magu amegawa vifaa tiba
vyenye thamani ya shilingi milioni 14 kwa Hospitali ya Wilaya ya Magu
pamoja na mitungi ya gesi 100 kwa wanawake wajawazito.
![]() |
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mery Masanja akipokea pongezi kutoka kwa Mganga Mkuu wav Magu mara baada ya kukabidhi vifaa |
Akizungumza leo katika hafla ya ugawaji wa vifaa hivyo vyenye thamani ya
shilingi 14,575,000 na mitungi ya gesi 100 kwenye Hospitali ya Magu, Mhe.
Masanja amesema vifaa hivyo vimetokana na mchango wake binafsi pamoja
na mchango wa Doris Mollel Foundation.
Amefafanua kuwa vifaa tiba hivyo vitasaidia kuokoa maisha ya watoto
waliozaliwa njiti na pia mitungi ya gesi itasaidia wanawake wajawazito
kupunguza shughuli nzito za kutafuta nishati mbadala.
Mhe. Masanja amewaasa wanawake wajawazito kuhudhuria kliniki mara kwa
mara ili kujua maendeleo ya mtoto anapokuwa tumboni.
Aidha, Mhe. Masanja amewataka wanawake wa Umoja wa Wanawake
Tanzania (UWT) kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada anazozifanya za
kuwaletea maendeleo wananchi wa Tanzania.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya ya Magu Dkt.Maria Kapinga
amesema vifaa hivyo vilivyotolewa na Naibu Waziri Masanja vitasaidia
kunusuru maisha ya watoto wanaozaliwa kabla ya muda ( njiti).
0 Comments