N Mwandishi wetu
Wanawake nchini wametakiwa kujiamini na kutoka mbele kupaza sauti zao ili kukabiliana na wimbi la vitendo vya ukatili vinavyowakabili. Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake, na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima alikutana na wananchi wa Kata ya Kirongwe alipotembelea eneo hilo hivi karibuni kukagua uundwaji wa Kamati za kupambana na ukatili wa wananwake na watoto wilayani Mafia.
Akionesha kutoridhishwa kwake na uhai Mabaraza ya Watoto na Kamati za MTAKUWWA hasa kwenye ngazi za Vijiji na Kata, Waziri Gwajima aliahidi kurudi wilayani Mafia na kupiga kambi ili aweze kuwafikia hadi wananchi walio katika visiwa vingine vidogo vidogo vinavyounda wilaya hiyo.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake, na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima (kushoto) akipokea taarifa ya utekelezaji wa vikundi vya kutokomeza ukatili kwa wanawake na watoto kutoka kwa Afisa Elimu Kata ya Kirongwe Bw. Venant Mwakalindile.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake, na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima (kushoto) akimpongeza mama Fatuma Mshangama Kombo kutokana na ujasili wake wa kupambanua uhalisia unavyoendelea katika jamii na umuhimu wa kuwepo kwa Kamati imara za kutokomeza ukatili kwa wanawake na watoto.
Awali, Mhe. Dkt. Gwajima alipokea taarifa kuwa matukio yanayoongoza kwa wilaya ya Mafia ni; ubakaji, ulawiti, mimba za utotoni na mashambulio ya aibu. Kwa Mwaka 2021/2022 jumla ya matukio 493 yalitolewa taarifa katika Ofisi za Ustawi wa Jamii na kituo cha Polisi ambapo matukio 56 yalikuwa ya ubakaji na ulawiti, kutelekezwa 64, shambulio la mwili 134 na shambulio la aibu matukio 239. Kati ya kesi hizo zilizotolewa taarifa, kesi 53 zipo Mahakamani na kesi 4 wahusika wamefungwa ambapo mmoja amefungwa maisha, kesi 5 wapo katika kifungo cha nje, kesi 11 zimekosa ushahidi na kesi 9 zinaendelea.

0 Comments