Na Shushu Joel, Kisarawe
MBUNGE wa viti maalum kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani Bi Subira Mgalu amewapatia vyerehani 20 Jumuiya ya Umoja wa Wanawake (UWT) Wilaya ya Kisarawe kwa lengo la kuinua uchumi wao.
![]() |
| Mbunge wa Mkoa wa Pwani wa viti maalum Subira Mgalu akikabidhi vyerehani kwa viongozi wa wilaya ya Kisarawe ( NA SHUSHU JOEL) |
Akizungunza na wenyeviti, Makatibu kata na viongozi wa wilaya mbalimbali wa jumuiya hiyo Mhe. Mgalu alisema kuwa ndoto yake kubwa katika uongozi wake wa ubunge wa Mkoa wa Pwani ni kuwaona Wanawake katika Mkoa huo wanakuwa kiuchumi ili waweze kufanikisha mambo yao pindi wanapokuwa na jambo lao.
Aidha alisema kuwa viongozi wanawake ni watu ambao wana umakini mkubwa pindi wanapopata dhamani ya kuongoza jamii kwa mfano Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan.
"Wanawake wa Pwani ni wachapakazi sana hivyo wakiwa na vitendea kazi kam hivi nilivyowafanikishia leo hapa kisarawe naamini wanakwenda kubadilisha maisha yao" Alisema Mhe. Mbunge wa Mkoa Mhe: Mgalu
Aidha Bi, Subira Mgalu amewataka wanawake kuanzisha viwanda vya ushonaji ambavyo watatoa ajira kwa makundi mengi pia kuongeza pato la Taifa kwa kulipa kodi mara baada ya kukua kwa mitaji yao kupitia vyerehani hivyo.
Mbali na vyerehani hivyo Mhe: Mgalu amewakumbusha wanawake wa wilaya ya kisarawe kuendelea kuyasema mazuri ambayo yanafanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwani kisarawe imefanikiwa kupata fedha nyingi kwenye miradi ya Afya, Elimu, Maji, Miundombinu na Umeme.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa UWT wilaya ya Kisarawe Asia Madima amemshukuru Mbunge wa Mkoa wa Pwani Bi Subira Mgalu kwa jinsi ambavyo amekuwa akipambana kuwainua wanawake kiuchumi.
Hivyo amemtaka kuendelea na moyo huo wa kuwa na kiu ya wanawake katika Mkoa wa Pwani kuwaona wanainuka kiuchumi kweli Mgalu ni Mbunge wa kipekee ambaye tunapaswa kumlinda kwani ni mboni yetu wanawake wa Pwani.
MWISHO


0 Comments