Na Asha Mwakyonde,Dodoma
WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imekabidhi vifaa vya kujikinga na UVIKO-19 Mikoa 12 ya Tanzania Bara na 5 ya Zanzibar lengo likiwa ni kuwakinga watoa huduma za afya hasa katika utoaji wa matone ya Vitamini A nchini.
Vifaa hivyo vimetolewa na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC),kupitia shirika la Kimataifa la Nutrition International (NI), kwa lengo la kuwakinga watoa hulduma hao ambavyo ni Katoni 6000 za Barakoa (Mask) na Vitakasa Mikono (Sanitizer) lita 6000 vyenye gharama ya Milioni 57.
Akizungumza jijini Dodoma leo Januari 5, 2022 wakati wa kukabidhi vifaa hivyo kwa wawakilishi wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI na Ofisi ya Makamu wa Rais-Muungano na Mazingira Mganga Mkuu wa Serikali Dk.Aifillo Sichalwe amesema vifaa hivyo vitawasaidia watoa huduma za afya na wale watoa huduma za afya ngazi ya jamii (CHW).
Ameitaja mikoa 12 ya Tanzania Bara ambayo imepata vifaa hivyo kuwa ni Dodoma,Kagera,Mwanza,Geita, Morogoro, Kilimanjaro, Simiyu, Shinyanga, Tabora, Singida,Tanga na Katavi na ile mitano ya Zanzibar.
Dk.Sichalwe amefafanua kwamba mikoa mitano ya Tanzania Visiwani imeteuliwa kwa kuwa ilikuwa na ufanisi duni kwenye utoaji wa huduma za mwezi wa afya na msaada huo utasaidia kuimarisha kiwango cha utoaji wa huduma za matone ya Vitamini A kwa watoto wengi zaidi nchini.
"Serikali inaendelea kuwapatia vifaa hivi ili kujikinga na maambukizi ya UVIKO-19 kwa watoa huduma waliopo vituo vya afya lengo likiwa ni kuendelea kutoa huduma hizi kwa ufanisi pamoja na Kampeni ya utoaji wa Matone ya Vitamini A ambayo inafahimika kama Huduma ya Mwezi wa Afya na Lishe ya Mtoto," amesema.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Dk. Ray Masumo
ameeleza kuwa vifaa hivyo vitawasaidia watoa huduma za afya waliopo mstari wa mbele katika kutoa hudama hizo pamoja na ile ya Huduma ya mwezi wa Afya na Lishe ya Mtoto kwa kuwa malengo yake ni kuhakikisha ifikapo Mwaka 2025 watoto wote nchini wanafikiwa na huduma ya matone ya Vitamini A kupitia vituo vya afya vilivyopo nchini.
"Naishukuru Serikali ya Cananda kupitia Shirika lake la Nutrition International kwa kuendelea kuiunga mkono serikali yetu katika vita dhidi ya UVIKO-19 pamoja na changamoto nyingine za Kilishe," amesema Dk Masumo.
Naye Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Kimataifa la Nutrition International (NI) Dk.Daniel Nyagawa amesema wametoa vifaa hivyo kwa Serikali ya Tanzania lengo likiwa ni kuunga mkono juhudi mbalimbali zinazofanywa na serikali kwenye kupambana na UVIKO-19.
"Tutaendelea kushirikiana katika masuala mbali mbali yakiwemo ya Kilishe ambapo shirika hili limekuwa likiyatekeleza hapa Tanzania," amesema.
Akipokea vifaa hivyo kwa niaba ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mkurugenzi wa huduma za Afya Dk.Mwanahamisi Hassan amesema vifaa hivyo vitawasaidia watoa huduma za afya waliopo mstari mbele katika vita ya UVIKO-19.
Aidha anawakaribisha wadau wengine kujitokeza katika kuunga mkono jitihada zinazofanywa na serikali katika vita ya kujikinga na UVIKO-19.
MWISHO
0 Comments